Tafakari Kwanza Kabla ya Kukata Tamaa
Posted by Apolinary Macha on 16:37 with No comments
Kila uamuzi wako unapelekea matokeo fulani katika maisha yako yajayo. Bado hujakutana na maisha yako yajayo na aina ya mtu utakayekwepo lakini kwa sasa umebeba mwanga wa kutambua na kupanga maisha yako ya baadae. Umewahi kujiuliza je miaka ijayo utakuwa katika maisha yapi? Ni jambo la muhimu sana katika kutafakari. Ni jambo ambalo litakusaidia kuweza kuwa na mipango yako ya maisha. Lakini unaweza kufikia hatua ya kutaka kukata tamaa na malengo yako yajayo. Ni kipindi kigumu sana cha kufanya maamuzi.
Unawaza Kuacha Ndoto yako au Mpango Wako?
Kuna wakati kila mmoja anafikia hatua ya kutamani kuacha au kukata tamaa katika lengo ulilopanga kulitimiza. Lengo hilo linaweza kuwa na faida kubwa katika maisha yako ya baadae. Lakini kutokana na kuona ugumu wa mpango huo au kukutana na changamoto mbalimbali unaweza kufikia hatua ya kutamani kuacha kuendelea kuamini katika mpango huo. Wengi wanakata tamaa katika hatua hii.
Jambo la Muhimu Kutafakari Endapo Ukiwa Unataka Kukata Tamaa
Wakati unapanga malengo yako, ulikuwa na lengo ambalo ulikuwa unaliwaza. Lengo hilo lilikuwa la muhimu sana na ndio sababu ulikubali kupanga jambo lako. Tambua, katika kila mwanadamu aliyefanikiwa kutimiza malengo yake, aliwahi kufikia hatua ya kukata tamaa. Lakini kinachotofautisha wanadamu ambao wametimiza malengo yao na ambao hawajatimiza malengo yao, ni mazoea ya kutokata tamaa.
Ukianguka, inuka na endelea na safari!
Safari inaweza kuwa ni ndefu, lakini usikate tamaa. Changamot zipo ili kutufanya wanadamu tuzidi kuwa imara. Mwanadamu anayekuwa na msimamo na malengo yake bila kukata tamaa, ni mwanadamu anayejitambua. Jambo la muhimu ukiwa unataka kukata tamaa jaribu kufanya yafuatayo:
- Usifanye maamuzi ya haraka
- Tafakari umuhimu wa jambo unalopanga kukata tamaa
- Safiri au badilisha mazingira, hii itakusaidia kutuliza akili vyema
Kuna Wakati Kukata Tamaa ni Jambo Sahihi
Sio kila jambo linahitaji kushikiliwa sana, ni vyema pia kutambua kuwa kuna wakati ni muhimu kukata tamaa. Hii inatokea pale unapotafakari na kugundua kuwa kuachilia jambo ndio suluhisho. Baada ya kutafakari kwa pande zote mbili, kuangalia faida na hasara za jambo unaweza kugundua kuwa kuna mambo ambayo kuna faida kubwa ukiyakatia tamaa kuliko hasara zake.
Katika malengo yako, tambua faida za kila jambo na manufaa yake katika maisha yako ya baadae. Kisha weka nia ya kufuata kilicho sahihi katika maisha yako ya baadae. Unapofikia hatua ya kutaka kukata tamaa, chunguza faida na hasara za kukata tamaa. Kisha ukiona njia sahihi au suluhisho sahihi la jambo, lifuate. Tenda kilicho bora katika maisha yako ya baadae.
Categories: Furaha, Happiness, Jitambue, Jitambue Sasa, Mafanikio, Mafunzo, Mambo ya Muhimu, Mawazo, Ndoto na Malengo, Ujumbe
0 maoni:
Chapisha Maoni