Uliza nafsi yako na tafakari, "Mimi ni nani?"

Posted by Apolinary Macha on 19:16 with 3 comments


Wewe ni nani?

Wewe sio kazi yako unayofanya, wewe sio kundi la watu unalojihusisha nalo.
Wewe sio mawazo yako,
Wewe sio Akili yako,
Wewe sio mwili wako,
Wewe sio mtu mwenye furaha, huzuni, hasira wala shida kama unavyojifahamu,
Wewe sio tafsiri uliyozoea kuifahamu.


Wewe ni nani?
Wewe sio ambaye wazazi wamekuambia,
Wewe sio ambaye marafiki wamekuwa wakikuambia,
Wewe sio ambaye viongozi wa dini wamekuwa wakikuambia,
Wewe sio ambaye serikali imekuwa ikikuambia,
Wewe sio maelezo unayotumia kujielezea kuhusu wewe.

Achia mbali majina unayoitwa, maelezo unayojielezea kwenye mitandao kama Facebook au mitandao mingine ya kijamii.

Achia mbali jina lako, aina ya mtu unayejijua wewe ndiye, sifa ulizonazo, muonekano, asili, tamaduni yako au sifa ulizoandikiwa kwenye kitambulisho chako cha kazi au masomo,

Je unajisikiaje hivyo vyote ukiviachia mbali na kujiuliza wewe ni nani.

Nini kinabakia ukitoa mali zako, mwili, akili, shida, mawazo yako, imani yako, mazoea yako, tamaa zako, jina unalopewa na watu au unalojipa wewe, na sifa unazopewa na watu na sifa unazopewa wewe?

Wewe ni nani?

Kama wewe sio unachofanya,
Kama wewe sio unachofikiria,
Kama wewe sio unachopenda,
Kama wewe sio maelezo unayotumia kujitambulishia,
Je Wewe ni nani?

Tambua kwa kina...

Hauzuiliwi na mipaka ya mwili,
Wala wewe sio mapigo ya moyo wako,
Wewe sio Akili yako, mawazo yako na hisia zako,
Je kama wewe sio hivyo vyote je wewe ni nani?

Vuta pumzi taaratibu, hewa hiyo inaingia kwenye mapafu halafu inaingia kwenye kila seli ya mwili wako.
Funga macho, acha kuwaza, acha kuweka mawazo nje yako, hisi nafasi inayobakia iliyo kimya, na isiyo fikiria, waza, wala isiyokuwa na hisia yoyote kutoka kwenye milango ya ufahamu.

Kumbuka wewe ni nani, kumbuka hauna mipaka, mwili utakufa utauacha, jinsia yako nayo unaiacha, mali utakuwa nazo bali nazo utaziacha, hisia ulizonazo ambazo chanzo chake ni mwili wako nazo utaziacha mwilini, hasira na mawazo nayo yote utayaacha, sifa ulizopewa kama vile ulikuwa mchoraji bora au mwimbaji bora n.k nazo utaziacha kwani nazo zinategemea mwili mfano unaimba kwa kutumia mdomo lakini ukifa unauacha na huo mdomo na sifa zake ulizozizoea.
Je kama maisha yako ya hapa duniani yatakapoisha vyote hivi unaviacha...
Je wewe ni nani???



Wewe ni ufahamu unaofahamu vyote hivyo,
Jiangalie ndani yako kwa kina,
Wewe ni empty,hauna kitu
Wewe ni sehemu ya muumbaji,
Kila ukionacho, unachokiwaza, unachokitenda, na unachokizungumza kinawakilisha ulimwengu wa ndani yako.

Wewe na mimi ni kitu kimoja, lakini ni fahamu mbili tofauti zenye upekee na umoja

Tunachopaswa kufanya katika safari ya maisha ni kujijua na kujitambua nafsi zetu kwa undani na kuamka.


Asante.