Hadithi ya Pango na Uhalisia wa Maisha. Hadithi Yenye Mafunzo Kutoka kwa Plato

Posted by Apolinary Macha on 14:35 with No comments
Miaka za zamani kulikwepo na mwanafalsafa mmoja aliyekuwa anaitwa Plato katika tamaduni za wagiriki. Naamini wengi wanamfahamu Plato kama mojawapo kati ya wanafalsafa wakubwa walioweza kufundisha mengi Ugiriki na maisha yake kuheshimiwa kutokana na utambuzi wake juu ya falsafa na maisha kwa ujumla.
Plato
Plato Aliwahi kuhadithia hadithi moja. Hadithi hiyo aliielezea kwa kufafanua maisha kwa ujumla yapoje na mwanadamu na ulimwengu.

"Fikiria pango ambalo ndani yake kuna watu wamefungwa tangu walipozaliwa na maisha yao wamefungwa ndani ya pango hilo.

Wafungwa walio ndani ya pango na hawawezi kutoka wala kugeuka nyuma

Na katika kufungwa kwao wamelazimishwa kutazama ukuta uliokuwa mbele yao. Watu hao wamefungwa shingoni na nyuma na wala hawawezi kugeuka nyuma kutazama kilichopo nyuma lakini maisha yao wamekuwa wakitazama mbele tu na wameshazoea na hawafahamu tena kama kuna kugeuka nyuma.
Wafungwa waliofungwa na kuutazama ukuta maisha yao yote wakiishi kuutazama ukuta, mwanga hafifu wa moto uliopo nyuma yao, na wakisikia sauti za wapita njia bila wao kuwatambua wala kutambuliwa.

Nyuma yao kuna moto unawaka. Na katikati ya moto ule unaowaka muda wote na pango wafungwa walipo kuna barabara inayopita kwa juu. Na fikiria kila siku kuna watu mbalimbali wanaopita kwani barabara ile ilikuwa inakwenda sokoni. Wanapita watu wa aina mbalimbali, mizigo na wanyama au mifugo. Vivuli vyao vinaonekana kwenye ukuta ambao wale wafungwa wanautazama muda wote na kutengeneza aina mbalimbali za vivuli vinavyopita na vinaonekana ni vikubwa na wao hawafahamu chochote kuhusu kilichopo nyuma yao na moto ule una mwanga hafifu unaotengeneza vivuli vya vitu na watu wanaopita kwenye barabara iliyopo katikati ya mwanga wa moto na kuelekea kwenye pango la wafungwa.


Barabara ya kwenda sokoni iliyopo nyuma yao ambayo wapita njia wanapita bila kujua kuwa kuna wafungwa chini. Wapita njia hao vivuli vyao na vya wanyama na mizigo yao huonekana kwenye ukuta mbele ya wafungwa na sauti zao  na zikisisika na wafungwa bila kufahamu zimetoka wapi.
Fikiria maisha yao yote wao wanaona hicho ni kitu cha kawaida na hiyo ndio dunia yao. Maisha yao yote wanazaliwa wapo kwenye pango na mpaka wanakufa wao wanatazama projection ile tu na hawajui lolote mpaka wanamaliza maisha yao Vizazi na vizazi zinapita na kuona hiyo ni kawaida. Vivuli, sauti za wapita njia, sauti ya moto unawaka lakini hawajui vinapotoka bali hujua vile vivuli ndio chanzo.

Sasa fikiria endapo mfungwa mmoja akatolewa kwenye pango, anapowekwa nje ambapo kuna mwanga wa jua na yeye hajazoea ni lazima ataumia sana na itamchukua muda kuuzoea kwani maisha yake yote na vizazi vyake hakuwahi kuhimili mwanga kama huo. Na akiweza kuona atashangaa sana. Atagundua kuwa alikuwa hafahamu chochote na hakutegemea kufahamu hayo.

Mfungwa aliyeishi maisha yake yote kufungwa kwenye pango na kutazama ukuta tu akifanikiwa kuuona ulimwengu na maisha mengine ambayo hakuwahi kuyaona maishani mwake.

Fikiria mfungwa yule aliyefunguliwa akaamua kurudi kuwajulisha wenzie kuwa kuna dunia tofauti na hiyo, endapo akirudi kwa pale barabarani kwa juu na kuwaambia kuwa "Jamani geukeni" wenziye hawatamuelewa. Watabaki kushangaa kuwa wanasikia sauti lakini hawajui imetoka wapi kwani wanatazama mbele na pia watabakia kuona kivuli cha lijitu au kitu kikubwa kipo kwenye ukuta wanaoutazama na hawatafahamu wanaambiwa nini na nani.

Sauti yake itakuwa kama makelele, kivuli chake kitakuwa kama kinawakera muonekano wake au kitakuwa kinawachanganya kufahamu ni jitu gani hilo limetengeneza kivuli kwani hawawezi kugeuka nyuma wala hawafahamu kuna kugeuka nyuma.

Kivuli cha yule mfungwa aliyeweza kuona maisha mengine na sasa amekuja kuwaita wenziye lakini hawezi kuingia ndani bali amekaa naye kwenye barabara ya nyuma ya wafungwa na kivuli chake kuonekana mbele ya wafungwa wanaoishi kwenye pango na sauti yake kuwashangaza wenziye. Wenziye wanashindwa kufahamu mwenzao anasema nini na wanamtafsiri katika uelewa wao wa maisha yao na picha waonazo kwenye ukuta ndani ya pango

Na pia endapo akipewa nafasi hata kushuka kwenye pango chini na kuongea na watamuona kama amechanganyikiwa kwa ambayo atakuwa anawaeleza kwani wao hawakutegemea kabisa. Pia itawachukua muda na wao kuzoea mwanga wa nje kwani walizoea giza. Na inaweza kupelekea hata wakamuona yeye ni tofauti na wao na kumshangaa au kumtukuza.

MAANA. 


Mpaka leo limebaki kuwa ni fumbo japokuwa wengi wamekuwa wakijaribu kutafsiri Plato alikuwa anamaanisha nini alipokuwa akielezea uhalisia wa mwanadamu. Fumbo hilo kila mmoja anaweza kulifikiria kivyake na kujitahidi kujitoa katika pango na kuweza kujitambua zaidi.



VIDEO YA HADITHI HIYO.