Maamuzi matatu yanayoweza kukufanya uwe na furaha.
Posted by Apolinary Macha on 19:34 with No comments
"Kuwa na furaha sio lazima uwe na vitu fulani, mali au raha kama wengi wanavyofikiria bali kuwa na furaha ni maamuzi ya mtu. Muda unaokubali kuwa na furaha na furaha nayo inakujia na kukufuata kama kivuli chako"
Kuachia sauti ya nafsi kufanya maamuzi.
Kuna wakati unashindwa kufanya maamuzi katika maisha, na wakati huu unakuwa ni mgumu kwani maamuzi yanakuwa ni magumu na ukiangalia pande zote mbili ni vigumu sana kuchagua uamuzi mmoja na kuacha mwingine. Wakati huu ni wakati ambao unashauriwa usiwe na haraka sana ya kufanya maamuzi, bali unapaswa kuacha wakati upite na utaona baadaye uamuzi fulani ndio unakuwa rahisi kwako kuuamua. Au kuna muda unashindwa kusubiri wakati upite kufanya maamuzi kwani utachelewa kufanya maamuzi, ni vyema kuisikiliza sauti ya nafsi yako. Chunguza kila uamuzi unaotaka kuufanya na kisha angalia faida na hasara za kila uamuzi. Ndipo ufanye uamuzi sahihi.
Kutambua kuwa FURAHA ni maamuzi ya mtu na sio HALI.
Watu wengi wamekuwa wakifikiri kuwa ili uwe na furaha ni lazima uwe na kitu fulani labda mali, muonekano, hisia n.k. Huu ni mtazama duni kwani unaweza kuwa na furaha hata kama usipokuwa na vitu hivyo. Kuwa na furaha ni maamuzi ya mtu, ukitazama kwa kina kuna watu ambao umewazidi mafanikio au mali lakini wana furaha zaidi yako, kama kuna mtu mwenye kidogo zaidi yako na ana furaha basi jiulize ni kwanini hauna furaha? Kumbuka wakati unapoamua kuwa na furaha bila kujali mali ulizo nazo, shida ulizo nazo utaona mabadiliko makubwa katika maisha yako. Utakuwa umeruhusu miujiza ya mabadiliko kuanza kwako.
Kukubali kuwa hujaja na chochote maishani na hutaondoka na chochote.
Wengi wamekuwa wakitafuta furaha nje yao. Wanadhani furaha inapatikana kwa mali, umaarufu, tamaa, hisia n.k. Lakini wapo wenye vyote hivyo lakini bado wana furaha sawa na wasio navyo na pia wanafariki na kuacha vyote. KInachojalisha sio raha na mali zako bali matendo yako. Tambua kuwa maisha ni kwa ajili ya kujitambua na sio kuja duniani na kukusanya mali za dunia. Walimu wengi wa imani wamekuwa wakituhimiza kuwekeza katika mali ambazo haziwezi kuibiwa wala kunyang'anywa na wezi wa dunia hii, bali kwa matendo mema, kujitambua na kuishi katika haki tunakuwa tumeweza kutimiza nafasi yetu hapa duniani ambayo ni ya mapito.
Tambua kila hali ina sababu yake, hali yoyote uliyonayo shukuru kwa kila jambo, na weka malengo ya hali ambayo ungependa uwe nayo. Kumbuka mawazo, matendo na maneno huumba hivyo simamia matendo yako, mawazo yako na maneno yako kuhakikisha unatumia hivyo katika haki.
0 maoni:
Chapisha Maoni