Kujitambua ni Hatua

Posted by Apolinary Macha on 18:23 with 1 comment



Katika kutambua mzizi wa matatizo yetu, tabia zetu, maisha yetu na ukweli wa maisha, kujitambua ni jambo moja la msingi sana. Mwanadamu hata akitambua kuna sayari ngapi, jua ni nini, nyota zote, na viumbe vyote; bila kujitambua mwenyewe, hawezi kuwa na hekima sahihi. Na pia kujitambua ni kitu kigumu, kujifahamu na kuona uhalisia wako inahitaji juhudi sana. Ijapokuwa inahitaji juhudi, ni jambo la muhimu sana kwenye maisha yako. Itakusaidia kuishi na watu, kutenda yaliyo sahihi, kuwaza yaliyo sahihi na kuwa na hekima katika maisha yako. Mtu anayejitambua na kufahamu kwa kina nini maana ya maisha kwake, tayari anakuwa amepiga hatua kubwa. 

Lakini katika kujitambua kunahitaji kutoa mawazo ya watu kwa jinsi wanavyokuelewa. Inahitaji kujitenga na vile ambavyo havina manufaa kwako, kufahamu akili yako vyema, kufahamu mawazo yako vyema. Na hii ni kwa hatua moja baada ya nyingine. 

Kujitambua ni kitendo cha hatua na hakina mwisho. Ni safari isiyo na mwisho. Kujifahamu vyema katika kila wakati uliopo, kuwa makini na akili yako na matendo yako, kuwa makini na mitazamo yako na kuishi katika njia sahihi inayokutenga na mabaya. Kufanya hivyo kutapelekea kuishi katika hekima, kuacha mabaya, kuwa mnyenyekevu, mwema, na kuishi katika kusudi sahihi la uumbaji.