Uhalisia wa Furaha na Mateso katika Maisha
Posted by Apolinary Macha on 18:25 with No comments
Maisha ni fumbo kwa kila mmoja wetu, na kila mwanadamu anaishi kwenye ulimwengu wake katika maisha yake. Fumbo la maisha ni kubwa na haijawahi kutokea mwanadamu ambaye ameweza kutoa mwanga kuhusiana na fumbo la maisha na jinsi ambavyo falsafa mbalimbali zimekuwa zikielezea. Ni fumbo ambalo tangu maelfu na mamia ya miaka iliyopita mwanadamu amekuwa akiwaza na kujiuliza kuhusiana na maisha ni nini. Ugumu wa swali hili ni kuwa kila mwanadamu anatafsiri kivyake na imani na falsafa ni nyingi na kila mmoja ina wafuasi wake. Unapokuwa falsafa ina wafuasi ni lazima kuwa kila mfuasi ameguswa na elimu hiyo na kuna sababu ya yeye kufuata maelekezo hayo na kujifunza kuhusiana na elimu hiyo au elimu mbalimbali. Yafuatayo ni mambo machache ambayo nimekuwa nikitafakari kuhusiana na furaha na mateso katika maisha yetu wanadamu:
Furaha katika maisha
Kila mwanadamu anaitafuta furaha! Tunapokuwa tunasoma shuleni ili kufaulu mitihani ni kwa sababu kufaulu ni furaha, kupata kazi nzuri ni furaha, kuishi sehemu nzuri ni furaha, kuwa na vitu vizuri ni furaha, kuwa na familia nzuri ni furaha, kuwa na afya ni furaha, kushinda ushindani ni furaha, kuwa na amani ni furaha, n.k. Kila tunachofanya tunafanya ili tuwe na furaha. Kila jambo ambalo tunaliwekea jitihana ni kuwa na furaha na kupunguza mateso na taabu za dunia. Furaha katika maisha yetu ni sehemu ya muhimu sana na ndio maana tangu tulipozaliwa tulianza kwa kujifunza kulia kwa ajili ya kuashiria kutopenda hali fulani na tulijifunza kufurahi kuonyesha hali nzuri; kabla ya kujua kuongea mwanadamu anajua kutofautisha furaha na mateso/maumivu katika maisha. Kila jambo tunalotenda ni kwa sababu ya kupenda kufikia furaha fulani.
Maisha yana mateso yasiyoepukika
Japo katika maisha yetu sisi wanadamu, tunajitahidi kuifikia furaha fulani lakini pia kwa upande mwingine hakuna mwanadamu ambaye ana furaha 100%. Bado kuna mateso ambayo yapo katika maisha na hayawezi kuondoka kamwe. Mwanadamu lazima azeeke, magonjwa mbalimbali, maumivu, kuishi na watu ambao wanatukosesha furaha, miili kuzeeka, majanga ya mvua, vimbunga, matetemeko, wanyama wakali na viumbe ambavyo hatupatani navyo mfano nyoka, simba n.k. Bado mwanadamu lazima ajitume ili kuishi vyema, lazima kuteseka kupata kile ambacho tunataka, na pia kuna mengi ambayo sisi kama wanadamu hatuwezi kuvipata. Maisha yana mateso yasiyoepukika.
Ukitafuta furaha kwa njia ambayo sio sahihi utapata mateso na hutovuna furaha sahihi
Chunguza katika maisha utaona kuwa mwizi hana furaha, muongo hana raha, mtu anayependa kuzini kuna taabu ataipata au anaipata katika maisha yake tofauti na mtu asiyefanya hayo. Mtu anayependa kulewa sana, kutumia madawa ya kulevya, kuvuta sigara, kupenda wanawake, kuua watu, kupigana, n.k vyote hivi huleta FURAHA YA MUDA MFUPI, na pia huleta taabu na mateso baadae. Wanadamu wanatofautiana jinsi ya kuitafuta furaha. Kuna njia sahihi za kuitafuta furaha ambazo ni njia zisizodhuru mwanadamu mwenzako, na njia isiyodhuru afya yako, maisha yako au mazingira. Kuna njia mbalimbali za kuitafuta furaha, kuna mtu anaitafuta furaha kwa kulewa, kuna mtu anaitafuta furaha kwa kuzini na kupenda wanawake, yote ni kuitafuta furaha au raha fulani katika maisha.
Tangu uumbaji ulivyoumbwa, furaha iliwekwa katika mazingira ambayo ukiitafuta katika njia sahihi utaipata na ukiitafuta katika njia ambayo sio sahihi utapata pia mavuno yake. Ni kama asali kwenye ncha ya sindano.
Utofauti wa maisha
Maisha yapo tofauti kwa kila mwanadamu. Wanadamu wanatofautiana sana kwa namna ambayo wanayaishi maisha yao, mateso na furaha wanazopitia. Kuna wanadamu wanaoishi kwenye taabu sana na kuna wengine wanaishi kwenye raha. Sio kwa sababu maisha hayana usawa, maisha yana usawa. Kwa wale wanaofahamu sheria ya KARMA, inasema kila mwanadamu anaishi katika maisha ambayo yeye mwenyewe ndio amepelekea kuyaishi. Inawezekana amesababisha kuishi kama alivyo sasa katika maisha haya au inawezekana katika maisha yaliyopita kabla ya haya kuna aliyotenda na kupelekea kuishi maisha haya. Na pia matendo ya sasa ndio muamuzi wa maisha yanayofuata. Kila hali ambayo mwanadamu anapitia ni kwa ajili ya kujifunza na kurekebisha makosa yake. Hakuna mwanadamu mkamilifu na ndio maana ni mwanadamu. Ukishakuwa mwanadamu inamaanisha kinachopaswa ni kujifunza na kujirekebisha maisha yetu. Mwanadamu ndiye kiumbe pekee anayejua ufahamu wa juu zaidi katika maisha na ulimwengu kwa ujumla. Pia ndiye kiumbe peke yake ambaye anajitambua. Jinsi tunavyowaza, matendo yetu, maneno yetu na fikra zetu ndizo zenye maamuzi ya maisha yetu tunayoyaishi.
Nini cha kufanya katika mateso na raha za maisha?
Kama hapo awali inavyoonyesha kuwa kwenye maisha kuna raha na shida. Kila analofanya mwanadamu ni kujifunza na kufahamu maisha kwa ujumla na pia kuitafuta furaha (katika maisha haya au maisha yajayo baada ya kifo). Kila mwanadamu ni dereva wa maisha yake, na kila mwanadamu anavuna fikra yake na matendo yake. Nini cha kufanya ili tuweze kuishi kwa furaha?
Kwanza ni kutambua kuwa kuna furaha ambayo inaweza kupatikana mfano kufanya kazi kwa bidii na kusimamia biashara zako vyema kwa ajili ya kupata kipato ambacho kitakusaidia kujikimu na kupata mahitaji ya muhimu kama sehemu nzuri ya kuishi, familia nzuri na mahitaji mazuri.
Pili, kuna ambavyo ni nje ya uwezo wetu katika kuwa na furaha. Mfano ni lazima mwanadamu afariki, watu wako unaofahamiana nao wanaweza kufariki, unaweza kuumwa ugonjwa wowote, unaweza kupata janga ambalo ni nje ya uwezo wako. Bado mwanadamu anazeeka, anakufa, anaumwa n.k Vyote vipo nje ya uwezo wetu na kila mwanadamu anapitia mateso fulani ambayo hana dawa ya kuyaondoa mateso hayo. Ni vyema kutambua hilo na halipingiki kabisa.
Tatu, ili kuwa na furaha katika mambo ambayo ni nje ya uwezo wako kama kuumwa, kifo, uzee; kwanza ni kutambua kuwa mateso duniani yapo, na kuna mateso ambayo ni nje ya uwezo wetu. Mateso haya hayaepukiki bali yanahitaji uwezo wako wa kutambua kuwa furaha inatoka akilini na sio kwenye hali uliyonayo. Unaweza kuwa na mateso yasiyoweza kuondoka wala kutibika na bado ukawa na furaha.
“Furaha katika maisha tunaitafuta, lakini pia kwenye maisha kuna mateso yasiyoepukika. Mateso haya ni sehemu ya maisha na mwanadamu anapaswa kujifunza kuitafuta furaha ndani mwake kabla ya kuitafuta nje yake.”
0 maoni:
Chapisha Maoni