Mambo 40 ya Kukufanya Kuendelea Kuwa Hai

Posted by Apolinary Macha on 17:11 with No comments


Wakati nilipoamua kukaa na kuandika hii mada, nilikuwa ninawaza "Ni mambo gani ya muhimu sana ambayo sijayatazama katika kunipa furaha". Kiukweli kuna mambo mengi ambayo watu wengi hawapendi kuyatazama au kuyapa kipaumbele. Mambo haya ni mambo ya hobbies, kazi, safari, au shughuli mbalimbali ambazo tunazifanya katika kuongeza furaha na kutufanya tutambue kuna kuishi.  Ambazo kila siku tunakuwa na nafasi ya kuvitekeleza katika kuwa na furaha.

Tuna mengi ambayo tumepanga kufanya katika maisha yetu, na mengi tunakuwa na mipango mbalimbali na kuna muda mengine hatutekelezi katika maisha yetu. Na mipango mingine ni sehemu kubwa katika kutufanya tuishi na kuyaona maisha kwa ujumla, ni katika kupata ile raha na furaha ya kuishi. Nimejaribu kutazama mambo mbalimbali ambayo wengi tumekuwa tukiyakimbia na kuogopa kuyatenda wakati kumbe vingeweza kutupa furaha katika kujaribu maisha yetu na kutufanya tupige hatua moja mbele.

Uhuru wa kuongea na kuonyesha hisia zako

Mimi binafsi sio mpenzi wa kuzungumza sana katika maisha yangu na inatokana na kuwa "Introvert" mtu mwenye tabia ya kupenda upeke yake na kutopenda kuongea sana. Lakini hata kama ni introvert kama mimi au extrovert, kuna mambo mbalimbali unayoweza kujaribu kusema na ukajifunza au kupata faida fulani kwako; Mfano:


  1. Mwambie mtu kile ambacho unaogopa kusema badala ya kubaki kusubiri mpaka yeye aseme.
  2. Mwambie mtu kile unachotaka kusema badala ya kubaki ukinung'unika
  3. Kubali kuonyesha kuwa una wasiwasi hata kama ni sehemu yenye watu wengi
  4. Mwambie rafiki yako ndoto zako na msikilize mawazo yake na kisha yachambue
  5. Kubali kumwambia rafiki yako jinsi unavyoutumia muda wako kisha jitafakari jinsi unavyoutumia muda wako na jifunze kuutumia vyema kwa sababu utaonekana unapoteza muda
  6. Jitambulishe kwa mtu ambaye unamuogopa au kujisikia wasiwasi kuonana naye
  7. Uliza rafiki yako kama kuna kitu unaweza kumsaidia
  8. Mwambie Boss wako au msimamizi wako wa kazi kile ambacho ungetamani angefahamu kuwa unaweza kufanya na malengo yako bila kusubiri yeye akupangie
  9. Usiogope kumwambia boss wako kuwa unaondoka pale unapokuwa unataka kuacha kazi
  10. Jiambie ukweli na usijidanganye hata pale unapokuwa umeshindwa kutekeleza jambo

Jaribu chochote ambacho umekuwa unatamani kufanya

  1. Tafuta chochote ambacho ulikuwa unapenda kujifunza mfano muziki, kupiga kifaa cha muziki, kuchora n.k 
  2. Kama huwezi kupata darasa jaribu kusoma na kuona video mbalimbali mitandao za kujifunza
  3. Muombe rafiki yako akufundishe kile ambacho anajua na ungependa na wewe kufahamu
  4. Jiunge na sehemu ya kufanya mazoezi kama una malengo bila kuogopa muda au kushindwa
  5. Tazama video YouTube kujua jinsi ya kutumia kifaa ambacho ungependa kufahamu
  6. Fikiria ni kitu gani ambacho ungependa kujifunza na leo jaribu tu hata kutazama mitandaoni na kujifunza hata somo dogo tu
  7. Andika Blog au Diary kujifunza kuwa mwandishi wa mawazo yako
  8. Nenda uwanjani kacheze mchezo wowote ambao ungependa
  9. Kila siku sikiliza mziki mmoja ambao unaupenda na ucheze kwa uhuru
  10. Andika listi ya vitu ambavyo ungependa kufanya na kufurahia kisha weka malengo kila mwezi utimize angalau vitano

Kusafiri na kutembea

  1. Panga sehemu ambazo ungependa kuzitembelea na weka malengo
  2. Kama huna uwezo wa kwenda anza kuhifadhi kiasi kidogo na anza kusafiri zile sehemu ambazo ni rahisi
  3. Nunua tiketi na ukizitumia tafuta utaratibu uzihifadhi kama kumbukumbu yako
  4. Safiri nje ya mji wako hata siku za wikiendi au likizo
  5. Tazama picha na video za maeneo ambayo ungependa kutembelea
  6. Mkaribishe rafiki yako mkutane kwenye mgahawa au sehemu nzuri ili mpige story
  7. Kama kuna maeneo unayoogopa kwenda mfano hoteli anza kuhifadhi kiasi kidogo kidogo
  8. Andika listi ya maeneo ambayo ungependa kulala na kupumzika
  9. Andika mikutano na semina mbalimbali ambayo ungependa kutembelea na andika list ya mikutano kila mwezi
  10. Tafuta maeneo ya kwenda kutembelea kwa ajili ya picha, kukutana na marafiki

Fanya yale ambayo hukutegemea kama unaweza kuyafanya

  1. Andika sifa ambazo ungependa kuwa nazo (mfano kuwa mwandishi, mzungumzaji mzuri, msomaji mzuri) kisha changua moja na anza kujifunza mbinu mbalimbani na kutenda yale uliyojifunza
  2. Kuwa karibu na rafiki anayekusaidia kuondoa wasiwasi wako na mwenye akili pana ya uhuru
  3. Andika maneno ya kuyarudia katika kujikaririsha jambo (mfano Mimi ni jasiri, Nitafanikiwa,) ambayo yatakupa moyo, ujasiri na kujiaminisha
  4. Mtafute mtu ambaye unamkubali sana kisha andika sifa ambazo unahisi yeye anazo ila wewe hauna hizo sifa na kisha jiwekee nia ya kujifunza
  5. Fikiria kitu kikubwa sana ambacho unatamani ungeweza lakini una wasiwasi kuwa huwezi kisha tenganisha hicho kitu katika majukumu madogo madogo kufikia hilo lengo kubwa
  6. Muulize rafiki yako akuelezee anavyokuona kisha andika ambacho unaona unapaswa kubadili na kile ambacho unapaswa kuendelea kuwa nacho. Hapa tafuta rafiki mwenye uhuru na anayeweza kukuambia ukweli.
  7. Kila siku andika kile ambacho kinakuogopesha au kukuumiza na baadaye tazama na chambua kwa umakini kila kitu
  8. Tafuta kile ambacho ungependa kujaribu kabla haujafariki, Tafakari maisha ni mafupi na nini ambacho ukiambiwa utafariki kesho utatamani kukijua mapema kabla haujamaliza safari yako
  9. Jitazame na angali mazoea ambayo hayana umuhimu na kisha jifunze kuyaondoa
  10. Tambua vile vinavyokufanya uwe na furaha na kisha endelea kuviweka na kujifunza zaidi. 

Kila mtu ambaye mpaka sasa yupo hai ana nafasi ya kuishi na kuyatekeleza yale ambayo anayapanga na kuweka nia yake. Kila siku jitafakari, na tazama maisha kwa upana. Maisha ni fumbo na hakuna anayeifahamu kesho, hivyo basi ishi na jifunze kila mara, tumia maisha yako kuandika historia yako ambayo utaiishi wewe na kuiacha wewe. 

Asante na endelea kuwa na furaha daima.