Ulimwengu wa Mitandano ya Kijamii kwa Watu Wenye Mahusiano

Posted by Apolinary Macha on 12:36 with No comments


Tunaishi katika Ulimwengu ambao ni tofauti kabisa na zamani. Mitandao ya Kijamii imetawala na imechukua nafasi kubwa katika maisha yetu, vyombo vya habari na mazoea ya kila mmoja. Hivi sasa kutokuwa na WhatsApp, Insta au application kadhaa inaonekana kama umejitenga kabisa katika mitandao na ulimwengu kwa ujumla. Dunia hii ya sasa watu wameweza kuwasiliana hata wakiwa mbali, kuonana katika call ya video, na watu ambao wasingeweza kuonana au kukutana wanakuwa marafiki. 

Kila jambo lina faida na hasara zake, kuna mambo mbalimbali ambayo tungependa leo tuyajadili katika kutazama maisha ya sasa na mitandao ya kijamii. 

Mahusiano ya Mitandaoni

Kupitia mitandao ya kijamii watu mbalimbali wameweza kukutanishwa na kuwa na mahusiano na mengine yameweza kabisa kudumu na kufika mbali. Ni wazi kuwa mitandao imeweza kusaidia hasa wale ambao walikuwa ni watu wakimya, wasioweza kuongea au kutoka na kukutana na watu mbalimbali. Pia kuna ambao wametumia mitandao kwa lengo la kuwatumia watu vibaya kimahusiano mfano kuwadanganya watu, kukutana nao na kutumia Fursa hiyo kimapenzi au kwa kuwatapeli. Hiki ni kipindi kigumu kwa sababu unayekutana naye huwezi kujua ametoka wapi, historia yake iliyopita na maisha yake kwa undani kwa sababu mtu anaweza kudanganya maisha yake katika mitandao. Kimekuwa ni kipindi kigumu sana kwa sababu ni vigumu kujua kila mtu kwa undani. 

Wivu na Wasiwasi

Matumizi ya mitandao ya kijamii pia yamepelekea kuwepo kwa wasiwasi mwingi na wivu katika mahusiano mengi kutokana na mwingiliano na urahisi ulipo katika mitandao. Facebook waliwahi kufanya utafiti mwaka 2017 kwa watumiaji 205 ambao walikuwa wanatumia Facebook. Ilionekana ndani ya mwaka mmoja asilimia 80% walikutana na hali ya wivu na wasiwasi katika mahusiano. Hii inatokana na uwezo uliopo wa kuwakutanisha watu mbalimbali kama vile wapenzi wazamani, marafiki wa mitandaoni ambao wana nia ya kimahusiano, marafiki wanaojaribu kuwa karibu na mwenza wako. Mitandao ya kijamii imepelekea watu kuweka maisha yao, picha zao, mada zao na interest mbalimbali ambazo huweza kupelekea kuvutia watu na baadhi ya watu kuanza kuwa wasumbufu kutaka mahusiano hata kwa mtu ambaye tayari ana mahusiano. Ni wazi kuwa wivu ni kawaida kwa mwanamke aliyeweka post yake akiwa amevaa nduo za kumuonyesha na kuna wanaume wana-like na ku-comment. Asilimia kubwa ya watu bado wanaweza kuwa na wasiwasi au wivu kwa marafiki wa jinsia tofauti na mwenza wake na wenye nia ya kutaka kumzoea sana. Na pia inaweza kumfanya mtu ajisikie vibaya pale anapoona ametuma ujumbe kwa mwenza wake na hajajibiwa lakini anamuona yupo online (kwenye mtandao huo huo au mwingine) au ame-post katika mitandao picha zake huku akiwa anachelewa kukujibu au kukutafuta. 

Usumbufu

Mitandao japo imeweza kuunganisha watu hata walio mbali, lakini kwa wale ambao Wapo karibu kuna ambao imekuwa ikiwaharibia na kuwaletea usumbufu hasa pale wanapokuwa pamoja. Jaribu kutafakari unazungumza na mwenza wako lakini yeye yupo kwenye mitandao anatazama mada mbalimbali na picha za watu. Mitandao inaweza kupelekea kero hata kwa watu mbalimbali ambao wanakufuatilia au marafiki wenye nia ya kukutaka kimahusiano au kumtaka mwenza wako. Pia Usumbufu mwingine ni kushindwa kufanya shughuli za kawaida za kimahusiano mfano kuzungumza pamoja, kula Chakula cha pamoja au kutumia muda kuwa na watoto. 

Kutambulisha Mahusiano

Ukitaka kufahamu kuwa pale unapowatabulisha marafiki zako kuwa mwenza wako ni nani, mfano nenda Facebook andika upo kwenye relationship na Kisha weka jina la mwenza wako, utaona matokeo yake ni makubwa na wengi huanza kukufuatilia katika mahusiano yako. Kwa wengine mahusiano wameweka usiri kuepuka usumbufu huu na wengine wamekuwa wakitumia vyema mitandao ya kijamii kuweka mada mbalimbali za wenza wao mfano kuwatakia siku njema katika siku zao za kuzaliwa, kuwashukuru, au kuonyesha upendo wako kwao. Ni wachache walioamua kuonyesha mahusiano yao na Wengi wamekuwa wakiyaficha hasa wale ambao wanahofia usumbufu, wasiri au ambao hawapendi baadhi ya watu kufahamu kama vile wazazi, wapenzi wa zamani au ndugu ambapo wangeleta mada nyingine ya kuuliza ni nini kinachoendelea. 


Ni wazi kuwa mitandao ya kijamii ni mizuri, imesaidia mengi na kusema tusiitumia itakuwa sio sahihi. Jambo la msingi ni kila mmoja kuweka mbele mahusiano yake kwanza kabla ya mitandao. Kuwa muwazi kwa mwenza wako, wasiliana vizuri na mwenza wako kabla hujawasiliana na wengine na mshirikishe vyema. Kwa wale ambao ni wasumbufu kukutaka wajulishe ukweli una mtu na jifunze kuwadhibiti. Sio jambo la hekima kusahau mahusiano yako kutokana na mitandao ya kijamii. Itaepuka kuondoa usumbufu, wivu, wasiwasi na kutumia muda kuwa na mwenza wako badala ya kujisahau kwenye mitandao ya kijamii katika ulimwengu huu mpya wa Mitandao na watu kuonyesha maisha yao.