Saikolojia ya Imani

Posted by Apolinary Macha on 20:09 with No comments

Imani ni jambo lenye nguvu na muhimu sana, linaloongoza jamii zetu, maisha yetu ya siku hadi siku, mawazo yetu, matumaini, mipango, na mahusiano. 

Unaposafiri kwenye ndege unakuwa na Imani kuwa ndege itafika, unapokuwa unajituma unakuwa na Imani kuwa utafanikiwa. Katika kila jambo tuna Imani juu yake na vitu vingine unavyoamini kwa sababu ya uzoefu: Mfano tuna uhakika kuwa Jua litakuja kesho asubuhi hadi sasa, kwa nini kesho itakuwa tofauti?

Lakini pia kuna mambo mengine unayoamini hata licha ya mantiki na ushahidi kinyume chake: Mfano kwenye tiketi za bahati nasibu. Pia kuna mambo ambayo tunayaamini lakini hatujajua kama tunaamini maana mara nyingi pia na ubongo unachambua mambo mbalimbali na kuyalinganisha na uhalisia ili kujua Imani yetu ipo wapi. Mfano mtoto anaweza kujua nguvu ya gravity bila kujijua, hata wakipiga mpira kwenda juu utaona wanausubiria mpira ufike chini. Mtoto hajui kama anaamini gravity ipo muda wote lakini katika upande wa ndani wa ufahamu (subconsciously) anaamini kuwa mpira utafika chini. 

Imani nyingine zinaanza pia katika familia unayokulia, mfano Imani za kidini, mitazamo juu ya jamii. Na kutumia milango yetu ya ufahamu tunajifunza dunia ilivyo na kutengeneza Imani mbalimbali juu ya vitu, watu na mambo mbalimbali tunayojifunza. 

Jonas Kaplan
Jonas Kaplan mtafiti wa neva na ubongo aliweza kuonyesha na kufanya tafiti inayoelezea mfumo wa neva unaojulikana kwenye ubongo kuhusiana na Imani na mitazamo mbalimbali. Hivi katibuni mwaka 2016 Scientific Reportwalitoa matokeo ya utafiti ambao watu walijitolea kufanyia uchunguzi wa picha za ubongo kwa kuangalia sehemu ambazo zilikuwa zinabadilika pale washiriki walipokuwa wanaambiwa wafikirie mawazo yao na kujadili mitazamo mbalimbali. Ilionekana kuwa pale walipokuwa wanafikiria Imani na mitazamo yao ubongo ulikuwa unaonyesha kuna neva kuna maeneo mbalimbali neva zake zilikuwa zinafanya kazi. Pia kifupi, pale mtu anapokuwa anawaza Imani au mtazamo mpya ubongo unaonyesha uwepo wa shughuli nyingi kwenye neva kuashiria kuwa kuna shughuli kubwa inaendelea. Watafiti hao pia walisema kuwa ni kutokana na shughuli ya ubongo kuhifadhi na kuchambua Imani mpya kwa kulinganisha na unachofahamu na unachoamini ili kuweka mtazamo mpya usiobadili sana kile ulichokuwa unaelewa mwanzo. 

Unapokuwa unaamini kitu, ubongo unatengeneza kumbukumbu na mara kwa mara huwa karibu na Imani hiyo. Pia pale Imani inapokaa sana inakuwa ni ngumu kubadilika na huamia katika upande wa uhalisia. Ni vigumu sana kutoa baadhi ya Imani hasa zile ambazo zimekuwa zikikaa akilini kwa muda mrefu, mfano kuamini kuwa kesho jua halitachomoza itachukua nguvu kubwa kuuaminisha ubongo hivyo. 

Watu wengi husema kuwa mtu anaweza kubadili Imani na mtazamo, ni kweli lakini inahitaji nguvu kuwa na sio kwa kusema unaamini kitu kipya tu. Kwa sababu muda unavyozidi kwenda ndipo Imani hujikita kwenye ufahamu wetu Zaidi na Zaidi.

Pia kuna wakati ni vigumu sana kuipinga mitazamo yetu na kuna wakati pale mtu anapokuwa anapinga Imani kuna wakati unajisikia vibaya ni kutokana na kuwa kubadili Imani ni kazi kubwa sawa na muda ambao ile Imani imekuwa ikikaa katika akili zetu. 

Cha ziada ni kuwa, kila Imani inapokaa katika akili zetu inapelekea mtazamo huo kuishi katika Maisha yetu. Imani inapokaa sana unakuwa uhalisia, na kile ambacho tunaamini kina matokeo makubwa sana katika Maisha yetu kwa sababu ndicho kinachoonyesha tunatazama vipi Maisha, tunachotenda na kila tunachofanya kwa kujua au bila kujua.