Kutenda Mema kuna Faida Katika Maisha haya ya sasa

Posted by Apolinary Macha on 15:52 with No comments


Kuna watu wanaamini kuwa tunatenda mema ili twende mbinguni au sehemu nzuri baada ya kifo. Ni wazi kuwa tunatenda mema kwa sababu vitabu vya dini vinatushauri kutenda mema na kutusisitiza kuwa ukitenda mabaya kuna adhabu yake baada ya mwisho wa maisha ya hapa duniani. Ni kweli, huu ndio mtazamo ambao wengi wanaamini. Lakini pia kwa mtazamo mwingine tunatenda mema kwa sababu kuna manufaa kwetu, watu wanaotuzunguka, viumbe vinavyotuzunguka, ndugu, na mazingira katika Maisha haya haya ya sasa hapa hapa duniani. Fikiria kama ingekuwa ni ruhusa kuua, kuiba au kufanya matendo ya kiovu bila kuwa na kosa, watu wengine ambao wangetendewa mabaya hayo wangekuwa wanapata taabu.
Mtazamo huu ni mtazamo ambao ni wa muhimu sana kwa kila mmoja, kwa sababu kwanza mwanadamu anapaswa kufikiria kuhusu kuishi maisha haya kiusahihi kwanza. Maisha baada ya kifo hatuna uhakika nayo wala kiukweli hatujui yapoje lakini cha msingi ni kuweka uzito kwenye maisha ya sasa. Katika Maisha haya ya sasa ni vyema kujua kuwa kila tunalotenda lina madhara kwa wanadamu wenzetu hivyo ni vyema tuishi vyema na tutende mema ili wengine na dunia iwe na Amani na watu wasiteseke.

Ukitaka kuamini kuwa matendo yetu yana madhara kuanzia katika Maisha haya, tazama kwenye maisha utagundua kuwa, kila mtu anayetenda mema anaishi kwa Amani bila taabu na wale wanaotenda Mabaya kuna taabu wanazipata. Mfano mtu anayelewa, mtu anayezini au mtu anayeiba, hawa wanapata taabu kuanzia katika maisha haya ya sasa na inaonekana katika maisha haya. Mfano kwa kupata magonjwa ya zinaa, magonjwa ya kutopendwa na watu, kupoteza mali, kutoendelea katika maisha n.k. 

Katika kuhakikisha safari yetu ya Maisha inaenda vyema ni sahihi kutenda mema kwani kuna matokeo sahihi ambayo tutayapata katika Maisha haya ya sasa kabla hata ya kifo.