Anza Kwanza Kupanda Mbegu sahihi Akilini na Kwenye Fikra yako

Posted by Apolinary Macha on 20:31 with 1 comment
Ni ukweli ambao haupingiki kuwa ulimwengu wa nje ni mfano wa ulimwengu uliopo ndani mwetu. Hii ni kwa maana kuwa maisha na kila kitu ambacho mtu anakiona kinatokea nje ya maisha yake ni kutokana na taswira iliyopo ndani yake. Tunaposema ndani yake, ni kwa maana ya kilichopo katika akili yake, imani, nia, upande wa ndani wa ufahamu na kumbukumbu kwa ujumla. Kwa wahenga hapo kale walisema "Aliwazalo mjinga ndilo linalomtoke" kuhusiana na kuunganisha mawazo na fikra kuwa ni chanzo kikuu cha matokeo katika maisha yetu.

Kwanza matendo yetu ni matokeo ya mawazo yetu, matendo yetu yanakuwa mazoea yetu, mazoea yetu ndio yanayotengeneza tabia zetu, na tabia zetu ndizo zinazochagua aina ya maisha kila mmoja anaishi. Hivyo basi kuanzia kwenye mawazo yetu mpaka kwenye matendo yetu, ni dhahiri kuwa matokeo yake hufika mbali sana na kutuchagulia matokeo mengi kwenye maisha yetu.

Hata katika vitabu vya dini mfano Zaburi inasema kama mwanadamu awazavyo ndicyo itakavyomtokea; na hata Yesu alipokuwa anatibu na kufanya maajabu kwa yule mtu aliyekuwa anamuamini kuwa akishika joho lake atapona na akapona kweli alimjibu, Imani yako imekuponya. Kwa upande wa Budha na imani za Asia nazo zinasema kwenye Dhammapada kuwa "Imani ya mwanadamu ndio mzizi mkubwa wa matokeo mengi katika maisha" ni kama kivule na mwanga.

Katika tafakari ya leo tujichunguze na kutambua ni nini ambacho tunakiamini, tunakifahamu, na tunachokitenda ili kujua matokeo tunayoyazalisha. Imani na Akili ni kama shamba, upandapo chochote, utavuna kile kile unachokipanda. Je unapanda upendo, amani, tabia sahihi? Au unapanda Hasira, chuki, masengenyo na uvivu katika maisha yako?