Sifa na Jinsi ya Kuishi na Watu Wanaopenda Kulalamika na Kutoa Lawama Sana

Posted by Apolinary Macha on 15:41 with No comments


Kuishi na mtu ambaye ana mitazamo hasi kunahitaji uvumilivu, lakini kuishi na mtu anayependa kutoa lawama kwa kila mtu ni vigumu sana. Mara nyingi katika jamii ambazo tunaishi, tunakutana na watu mbalimbali na kila mmoja anakuwa na tabia yake. Ni kawaida kwa kila mtu kukutana na mtu/watu wenye tabia ya kupenda kulalamika. Watu hawa hawakosi sababu ya kumlalamikia mtu. Mfano unaweza kumkuta anaperuzi simu yako na akakulalamikia kuwa ni kosa lako kuacha simu bila kuiweka pass-code. Anaweza akaangusha kitu na akakulalamikia wewe kwa kumfanya kupoteza umakini wake. Katika kila jambo anaweza kutafuta sababu ya kusema kuwa ni kosa lako. 

Watu hawa wanakuwa na sifa zifuatazo:

1. Hawawezi kukubali kosa lake binafsi

Katika kila jambo, watu hawa lazima watatazama kosa lako bila kutazama upande ambao na wao wanahusika. Hawawezi kukubali makosa yao, na hujichukulia kama wao ndio waadhirika zaidi wa tatizo. Wengine hawawezi kabisa kuomba radhi/msamaha kwa makosa ambayo wamekosea wao, kwa sababu hawaoni upande wao. Kutokana na kutazama makosa ya watu sana inafikia hatua hawawezi kuona na upande wao kwani wanatazama sana upande wa watu.

2. Hukufanya ujisikie vibaya

Katika kila wakati ambao mnakuwa mnaelekezana, ni vyema kuhakikisha kuwa unahakikisha mwenzako anajisikia vyema hata kama kosa ni la kwake. Watu wanaopenda kulaumu watu na kutoa lawama kwa kila mtu wanapenda sana kujiona wapo sahihi na hawapendi kusikiliza watu wengine. Hali hii ya kutopenda kusikiliza watu inapelekea mtu kujisikia vibaya. Kila mwanadamu anapenda kupewa nafasi ya kusikilizwa hata kama amefanya kosa. Kutokana na watu wa namna hii kutopenda kusikiliza watu na kujiona wapo sahihi zaidi ya watu wengine inapelekea mtu kujisikiza vibaya., 

3. Hawajalishi jinsi gani wanapelekea watu kujisikia vibaya

Watu wa namna hii hawajali utaumia au utawachukulia vipi. Wao kupenda kulaumu na kujitoa katika malalamiko na kuelekeza malalamiko kwa watu bila kujali mwenzake atajisikia vipi. Watu walalamishi hawaamini kabisa kuwa wanachofanya ni kosa na kuna wakati hichi kitendo kinapelekea wao kutotambua adhari ya tabia yao.

4. Huamini matendo yako ni sahihi zaidi

Watu walalamishi huamini kuwa wanachotenda ni sahihi zaidi na hupenda kuelekeza malalamishi kwa watu wengine. Hupendelea kuona walichokifanya wao ni sahihi na ulichofanya wewe ndio kosa.



Jinsi ya kukabiliana na watu wa namna hii

Kwanza tambua kabisa kuwa watu wa namna hii ni vigumu sana kuwabadili

Katika kuishi vyema na watu wa namna hii ni vyema kufahamu kuwa, watu wa namna hii ni vigumu sana kuwabadili. Kila mwanadamu ana mfumo wake wa kuishi na hii inapelekea kuwa ni vigumu sana kumbadili mtu. Pia kama ulivyoona hapo juu kuwa watu wa namna hii wana sifa ya kuona kuwa wanachofanya ni sahihi. Hivyo inakuwa ni vugumu sana kwa watu wa style hii kubadilika. Ili kukusaidia kuondoa mawazo kwanza tambua kuwa mtu wa namna hii haoni anachofanya sio sahihi na mara nyingi ni wagumu kubadilika. Pia kutambua hivyo kutakusaidia kupunguza mzozo na malumbano.

Katika chochote ambacho utajitahidi, kwao hawawezi kuona umuhimu wake.

1. Epuka kujitetea sana

Katika majadiliano na watu wa namna hii, epuka kujitetea sana na sikiliza wanachosema zaidi ya kujitetea. Ukiwa unazungumza au kuelekeza watu wa namna hii epuka kujitetea sana zaidi  ya kusikiliza. Baada ya kuwasikiliza, uliza nini cha kufanya kusuluhisha kila maliza majadiliano. Kama unatambua kuwa ni kosa lake, msikilize na mpe nafasi sana ya kujielezea na kisha gundua nini cha kufanya. Pia epuka kushambulia watu wa namna hii kwa maneno au kurudisha lawama sana. Na usiache kujitetea kwa sababu ni haki yako kumuelewesha, asiposikiliza achana kulumbana naye sana.

2. Usichukulie kila wazo lao binafsi

Kutokana na kuwa watu wa namna hii wengi wao wanapenda kutazama sana upande hasi na wanapenda kutoa lawama kwa kila mtu; wanaweza kuwa na maneno au mifano ambayo inakejeli, inaweza kukufanya ujisikie vibaya, inayokushusha dhamani, na bila kujali utajisikiaje. Ili kuweza kushinda hali hii, usichukulie kila kitu katika nafsi na jifunze kupuuzia baadhi ya mawazo yao ambayo hayana maana kuyaweka akilini. Hii itakusaidia usijisikie vibaya na ukawa na amani ya moyo bila kujali mtu wa namna hiyo amekuwa akikuzungumzia vipi.

3. Kuwa jasiri

Pia ili kuweza kuhimili watu wa namna hii, kuwa jasiri na penda kujiamini. Kama una uhakika kuwa wewe sio mwenye makosa na mtu wa namna hii anakutolea lawama bila kujitazama wewe, usiache kujitetea na kuelezea kuwa sio kosa lako. Kama asipoelewa ndipo achana naye badala ya kujitetea sana. Kuwa jasiri na kuwa na msimamo, itamfanya atambue kuwa na wewe una misimamo yako hasa pale unapotambua upo sahihi.

4. Epuka kuonyesha hisia zako sana

Watu wa namna hii wanapelekea mtu kuwa na hasira, na unaweza kukasirika sana. Ili kuepuka kuumia sana, hakikisha usionyeshe hisia zako sana na onyesha tabasamu. Usichukulie mawazo yao binafsi yakutawale akilini. Usikubali wapoteze furaha yako. Vaa uso wa tabasamu na usikasirike wala kuchukia kufikia hatua ya kufanya maamuzi ambayo sio sahihi.

5. Epuka mazoea sana na kuwa na plani nyingine za kufanya

Watu wa namna hii sio watu wa kuwategemea sana. Epuka kuweka mategemeo sana kwa watu wa namna hii na usiwape kipaumbele sana katika maisha yako kwa sababu hawategemeki na kuna wakati watakufanya ujisikie vibaya. 

6. Usikubali wakubadilishe

Kama unajua upo sahihi, usikubali ubadilike kwa sababu ya madhaifu yao. Kuwa na msimamo wako na simama pale unapotambua kuwa upo sahihi. Hata kama itafikia hatua ambayo itakubidi ukubali tu mawazo yao ili ukasirike, usikubali ndani ya moyo wako uchukie au kubadilika. 



Changamoto zao
Jinsi ya kuwakabili
Hujiona wapo sahihi zaidi 
Jielezee vyema na washikilize; epuka kupoteza nguvu yako kubishana
Wanaweza kukufanya ujisikie vibaya
Jiamini na simamia mtazamo wako. Pia jifunze kupuuzia mawazo yao yasiyo na umuhimu
Wanaweza kukufanya uonyeshe hasira
Tuliza akili na epuka kuonyesha hasira yako
Wanaweza kukushambulia kwa maneno na kukufanya ujisikie vibaya
Jifunze kupuuzia