Jinsi ya Kupanga Malengo katika Ndoto Yako ya Maisha

Posted by Apolinary Macha on 16:45 with 2 comments
Kuna tofauti kubwa kati ya ndoto na malengo. Ndoto ni ile picha uliyonayo inahusiana na wakati ujao. Mfano unaweza kuwa na ndoto za kuwa mjasiria mali bora, picha hiyo inakupa hali ya wakati ujao. Kumbuka ndoto inayozungumziwa sio ndoto inayohusiana na wakati ukiwa umelala bali ni ndoto ya picha na matazamio ya baadaye. Malengo ni mpango yako katika kufikia ndoto zako za maisha.
Kuna tofauti kati ya dreams and goals.
Watu wengi wana ndoto, na sio malengo. Na hii ndio sababu kuna watu wachache wenye malengo wanaoweza kutimiza ndoto zao kwa sababu ndoto ili itimie inahitaji malengo, na malengo hayo yafanyiwe kazi ili kufikia ndoto tarajiwa. Mfano wa tofauti kati ya ndoto na malengo ni: unaweza kuwa na ndoto ya kuwa mjasiria mali. Malengo ya ndoto hii ni kujituma katika biashara, kutumia biashara iliyopo kuongeza wigo wa biashara na kuongeza mahusiano na wafanyabiashara wengine. Ukitazama mfano huu utagundua kuwa malengo ni hatua ambazo mtu akiweza kuzifuata anaweza kufikia ndoto ambayo anaitarajia kwa hapo baadae.

Watu wengi hawawezi kutofautisha ndoto na malengo. Mfano mtu anaweza kusema ana ndoto ya kuwa na utajiri. Kuwa na utajiri sio malengo bali ni ndoto, kuwa wa kwanza katika masomo sio malengo bali ni ndoto. Malengo ni kile unachopaswa kufanya ili kufikia ndoto uliyonayo. Malengo huusisha tendo na kujituma kufikia ndoto au mpango fulani. 

Kupanga Ndoto - Ni kitendo cha kutafakari ndoto yako ya maisha kwa umakini wa juu. 


Jiulize kwa kutafakari; unapenda maisha yako ya miaka 5, 10, 20, na kuendelea ijayo uwe umefikia malengo gani. Andika kila picha na taswira unayoipanga na iwe ndio lengo lako kuu na utaridhika nayo. Andika kila maelezo bila kuacha taswira yoyote ambayo unaipanga. Inawezekana ikawa ni kiasi gani unapanga kuwa nacho, uwe na kazi ya aina gani, uwe unaishi wapi, uwe na biashara zipi, na uwe na tabia gani. 

Kupanga Malengo - Katika kufikia ndoto yako ni vyema kupanga malengo ambayo yatakusaidia kufikia malengo hayo. Katika kufikia kila lengo, hakikisha unaweka na malengo ya kufikia ndoto yako. 


Baada ya kupanga ndoto yako katika miaka ijayo, panga malengo yanayoendana na ndoto yako.

Andika kila unachopaswa kufanya na kufahamu ili kufikia malengo hayo. Andika kila kitu unachopaswa kufanya ili kutimiza ndoto zako za maisha. Kisha tazama "je inawezekana kufanya hicho unachopaswa kufanya?" Kama jibu ni ndio hakikisha unaanza kujizoesha kutenda kila unachopaswa ili kutimiza ndoto zako za maisha ambazo ulizipanga hapo mwanzo.


Kwa ufupi:
  1. Tafakari picha ya miaka ijayo na ambacho unatamani kutimiza na malengo unayopanga kufikia
  2. Chambua kila ndoto yako ya maisha inayoendana na picha hiyo
  3. Weka malengo madogo madogo ambayo ukiyatimiza kila mwezi, mwaka na siku itakusaidia kufikia malengo hayo
  4. Anza kufanyia kazi kila unachopaswa kufanya
  5. Utaitimiza picha yako.