Mwenza Wako Sahihi; Yupo Ndani Yako Kwanza.

Posted by Unknown on 09:04 with No comments


Katika miaka ya sasa wengi wamekuwa wakitafuta wenza wao wa maisha. Wengi wana mtazamo kuwa mwenza wako wa maisha ndiye atakaye kukamilisha, yaani hujakamilika mpaka umpate yule ambaye anakamilisha sehemu yako iliyobakia, na ndio maana wengine hutumia majina kama vile "Soul mates" na "Other Half". Wengi wanahisi hawajakamilika na watakamilika wakimpata mwenza wao wa maisha. 

Lakini, kila mwanadamu amekamilika. Wanaosema kuwa mpaka umpate mwenza wako wa maisha ndio umekamilika, wanaweza wakawa wapo sahihi katika kukupa picha ya kuwa mwenza ni muhimu lakini sio kwamba ukiwa hujampata basi hujakamilika au kama upo "Single" haujakamilika. 

Ukweli ni kuwa umekamilika kabisa, mengine yote ni ya ziada tu na sio lazima yawepo katika kukukamilisha. Ulipokuja hapa duniani ulikuja mwenyewe na utaondoka mwenyewe. Usijidharau na kujishushia cheo kwa kuona ambao wapo peke yao ni wapweke au hawajakamilika. 

Itafute furaha ndani yako. Tengeneza furaha isiyo na mategemeo kwa watu, vitu na hali. Furaha unayoitengeneza kupitia watu ni fupi, kwani watu wale wasipokuwepo utakuwa hauna furaha hiyo, watu hao wakitenganishwa na wewe kwa vifo, uzee, majukumu, kutokuwepo kwa maelewano, safari n.k furaha yako itapungua. Ukitengeneza furaha kupitia vitu siku ukivikosa furaha yako itapungua.

Simaanishi kuwa usishirikiane na wenzako au uwe mbinafsi, bali tunachomaanisha hapa ni kuwa; kabla ya kuitafuta furaha nje yako itafute kwanza ndani yako. Ukishaipata furaha ndani yako kisha itoe nje na wafanye wale ambao wanakuzunguka wawe na furaha. Hii ni aina pekee ya kuitengeneza furaha. 

Na pia kama una mwenza wako, mjali, mpe heshima yake, mthamini, na mpende kwa dhati. Wakati uliopo ni mfupi sana na hubadilika katika kila sekunde. Jitahidi kuutumia vyema. Tengeneza amani na upendo sahihi ndani na nje yako. Kama hauna mwenza wako basi jithamini na jipende. Jione umekamilika, siku nafasi itakapokufikia na kuweza kumuona anayekupenda basi itumie nafasi hiyo vyema. 
Categories: , , ,