Siri ya Kweli ya Kujipenda.

Posted by Apolinary Macha on 17:34 with No comments
Kujipenda na Jithamini kimwili na kiakili huongeza furaha yako.

Mwili wako ni chombo cha muhimu sana katika maisha yako ya sasa. Kwa kutumia mwili wako na sehemu mbali mbali za mwili tunaweza kuielewa hii dunia na ulimwengu kwa ujumla na pia katika kufurahia maisha. Japokuwa mwili sio sehemu yetu ambayo ni ya kudumu au yenye maisha ya milele kama vile ilivyo sehemu ya ufahamu, lakini katika safari ya sasa ni vyema kutambua umuhimu wa mwili wako na kuweza kuishi vyema bila kuukosea au kuutumia vibaya. Wengi wamekuwa wakitumia mwili vibaya katika matendo mabaya, na katika mawazo mabaya. 

Kuna faida kubwa katika kuuthamini mwili. Mwili usipoweza kuthaminiwa hata furaha ya mwanadamu haitapatikana. Mfano kama unautumia mwili katika matendo yenye hatari katika afya, unaweza kupelekea baadaye maisha yako yakakosa furaha kwani unaweza kupata matatizo kama vile kuumwa, kuishi na matatizo ya afya na kathalika. Hivyo katika kuitafuta furaha kwenye maisha ni vyema mwili kuujali kwani usipoujali utateseka na kupelekea kutopata amani na furaha hata hapo baadae. 

Kwanini tunasema ni vyema mtu kuujali mwili wake:

 1. Weka Umakini Katika Mawazo Yako. 
Kuna namna nyingi zinazoweza kuuathiri mwili mfano katika akili. Angali amawazo yako na fikra yako inautazama mwili katika hali gani? Je unatumia muda mwingi kuwaza matatizo ya mwili? Je unatumia muda mwingi kuulalamikia mwili wako? Wazo lolote linapelekea matokeo. Hivyo katika hatua za kuupenda mwili wako anza kuupenda akilini na ondoa mawazo duni.

2. Jitazame Jinsi Unavyojihukumu.
Kila mmoja kuna namna anayojihukumu. Unaweza ukawa unahukumu matatizo ya mwili wako. Unaweza ukawa unahukumu tabia na mazoea yako ambayo unaona yanakukosesha afya. Badala ya kuhukumu jifunze kubadilisha kile ambacho unaona sio sahihi.

3. Jikubali na Jiamini.
Baada ya kuwa makini na mawazo yako na fikra zako, jiamini. Jikubali na amini mwili wako umekamilika. Badala ya kuona mapungufu yako mfano kilema, ugonjwa, au tatizo ambalo huwezi kulibadilisha basi weka akili yako na jikubali kwa kutazama pale ambapo unaona pana ubora katika mwili wako badala ya kutumia muda mwingi kulalamika na kuhuzunika.

4. Chukua Hatua. 
Baada ya kuona kuwa kina kila hali ambayo unayo na kuchunguza tabia na mazoea ambayo unaona hayana umuhimu katika mwili wako basi chukua hatua. Badili pale unapoona ni pabaya. Chukua hatua za kujiimarisha kiakili na kimatendo. Kisha baada ya kuzingatia hayo utaweza kuishi kwa amani.

Siri kubwa katika kuupenda mwili wako na kuujali inaanza katika akili yako na kisha kwenye matendo yako. Kuna faida nyingi katika kujijali, kujitambua na kuthamini miili yetu. Kuishi katika mwili wenye matatizo, magonjwa, na mapungufu ambayo tumeyapelekea wenyewe katika mwili wetu, hupelekea mtu kukosa furaha.
 
Ni vyema kuheshimu miili yetu katika namna zote. Kiafya na kisaikolojia. Vyote hivi vitakusaidia kuishi katika maisha ya furaha na amani. 


Categories: , ,