Njia Tano za Kuacha Kutaka Kumridhisha Kila Mtu.

Posted by Apolinary Macha on 23:30 with No comments
Usikubali kukosa amani kwa kulazimisha kila mtu afurahi au akuelewe kama unavyotaka wewe.

Mojawapo ya ufahamu ambao wengi hufikia kuuelewa katika kuishi na wanadamu, ni kuwa katika maisha, sio lazima umridhishe kila mwanadamu. Pia sio lazima upendwe au kujaliwa na kila mwanadamu. Kuna watu ambao hawana amani mpaka wamfurahishe kila mtu, hupelekea kuwa na wasiwasi jinsi wanavyosemwa na wengine, kukosa amani pale wanaposhindwa kutimiza malengo fulani kwa watu, huwaza mitazamo ya watu inamtazamaje na wengine hupelekea kuamua kujilazimisha kufanya wasiyoyataka kwa lengo la kumridhisha mtu au kikundi cha watu.

Kinachozungumziwa hapa ni jinsi ya kutaka kulazimisha kila kitu kiende sawa kwa kila mtu anayekuzunguka. Unatanguliza hivyo na kujisahau kuwa unatakiwa ujijali kwanza wewe na kufahamu misimamo yako badala ya kutokuwa na misimamo kwa kutaka kuenda sawa na misimamo ya watu. Misimamo ya watu sio mibaya, ni vyema kuifahamu lakini kwanza ni vyema kuwa na msimamo wako wewe kama wewe ndipo utambue thamani yako kwanza badala ya kutokuwa na thamani yako wewe kama wewe.

Watu wasiojali misimamo yao na kutaka kuridhisha kila mtu hupelekea;
  • Kusema "Ndio" kwa wasiyoyapenda kwa malengo ya kuridhisha wengine,
  • Huweka mawazo sana muonekano wake ulivyo,
  • Hukosa amani hasa kwa mambo yaliyo nje ya uwezo wao,
  • Hutanguliza nia za wengine zaidi ya malengo yake,
  • Hudhindwa kukataa wasivyovipenda,
  • Hufikiria wengine wanamtazamaje,
  • Hukosa amani wakati anaposhindwa kutimiza ahadi.
Unaweza kujifunza kuacha kabisa hali ya kutaka kuridhisha kila mtu kwa kufahamu hatua hizi tano.

1. Kuwa na amani na tambua kuwa sio kila mtu atakupenda na kukujali, na hilo sio tatizo bali ndivyo hali halisi.

 Unaweza ukawa unaona ni lazima kila mtu akupende au akuelewe lakini kwanza tambua hakuna mwanadamu aliyependwa na wote. Hata mitume na manabii kuna waliowaona ni wabaya au waongo na kukataliwa na wengine. Sio kila mtu utakayekutana naye katika maisha atakuona sawa na unavyotaka wewe akuone. 

Hivyo cha kufahamu ni kuwa tambua thamani yako, ukishaitambua thamani yako ilinde na ifuate. Kama unajiepusha na zinaa, pombe, kusema uongo, kuwasema watu vibaya, unajituma na sio mvivu, hauui wala kuadhiri mtu wala maisha, hata kama ulimwengu wote usipokuelewa cha msingi fahamu msimamo wako unasimami wapi. Ni kuufanya moyo wako uelewe kwanza kabla ya kulazimisha moyo wa mwenzako uelewe.

2. Jifunze kukataa ambacho unakiona sio sawa kwako.

Unapotambua thamani yako ni nini, utailinda na kuhakikisha haipotei. Unapoona inakubidi kuharibu thamani yako kwa kuridhisha watu basi utambue kuwa sio sahihi kufanya hivyo. Thamani yako ni ya muhimu. Kama watu wameshindwa kukuelewa au kukufahamu kwa unavyotaka wewe hilo halijalishi, kinachojalisha unajithamini kiasi gani. Ukweli unao ndani mwako na haina haja ya kuutafuta ukweli kwa mitazamo ya watu.

Wengine hutenda vitendo wasivyovipenda kwa kushindwa kukataa kwani wanaogopa wataonekana wa ajabu au hawatamridhisha mtu au watu fulani.


3. Jifunze kutojutia pale unapokataa kumridhisha kila mtu.

Badala ya kuumi kwa kukataa jambo fulani linaloendana kinyume na dhamani yako, kubaliana na hali na usijutie. Pale nafasi nyingine itakapokuja ya kukupa nafasi ya kufurahisha mtu au watu bila kuharibu au kushusha dhamani yako itumie vyema. Ikija nafasi mbaya ikatae na usijutie. Weka msimamo na simamia msimamo wako daima.

4. Jifunze kuweka mipaka.

Jinsi watu wanavyokuzoea na kukufahamu ni kutokana na mipaka yako uliyojiwekea kipindi unaanza kuwafahamu mpaka sasa. Weka mipaka yako kwa kujali afya yako, akili yako, mwili wako, Imani yako, na hakikisha ni kwa manufaa mazuri. Mfano weka mipaka ya kula vyakula safi na bora, utakapokutana na mtu na kuanza urafiki naye mzoeshe mipaka yako aifahamu, mfano akikuambia tukale Chips Mayai unakataa kwa kumwambia kuwa unapenda kula vyakula vyenye afya na kumshauri na yeye ale chakula salama na mlo salama. Pia kama haupendi pombe unapokutana na marafiki wazoeshe kutokunywa nao watambue kuwa una mipaka yako. Hii ni mifano tu lakini katika maisha kila mtu ana hali anazozikuta na kuhakikisha anafanya maamuzi sahihi.

5. Kubali kuachana na watu wanaovuka mipaka yako.

Kama mtu anakulazima kufanya usichokipenda kwa malengo yake una haki ya kukataa, kama mtu hakupendi na umejitahidi kumjali achana naye. Bila kumchukia na bila kumkasirikia, kwa amani na upendo unapunguza mazoea sana na weka msimamo kwani hufanyi kwa ubaya bali unafanya kwa uzuri na usafi wa moyo. Wewe ndiye muamuzi wa kulea wanaokurudisha nyuma na wewe ndiye muamuzi unaweza kuwakataa kuwale.

Mwisho kabisa ningependa kusema kuwa, ni taabu sana kumfanya kila mtu afurahi na aridhike. Mwanadamu akiridhika na hichi atataka kile, na akikipata atatamani kingine. Cha muhimu ifahamu thamani yako na malengo yako ya maisha, yalinde na uyafuate daima. 

Asante.