Hadithi: Jinsi ya Kukabiliana na Mtu Anayekutusi au Kukejeli.

Posted by Apolinary Macha on 19:08 with No comments


Wengi tumeshapitia hatua hii ya kukutana na watu ambao ni wepesi kutukana, kudharau, kukejeli au kuhukumu watu. Ningependa kushare hadithi hii ya Kibuddha ili kila mmoja aielewe vyema.

Siku moja Buddha alikuwa anatembelea katika kijiji kwa ajili ya kufundisha Dhamma. Kulikuwa na kijana mmoja mwenye hasira na mkaidi katika kijiji kile akaanza kumtusi Buddha.

Akisema " Huna haki ya kufundisha watu" huku akisema kwa sauti na ukali. "Wewe ni mjinga kama watu wengine. Wewe ni muongo".

Buddha aliendelea kuonyesha amani, bila kukasirika. Akamuuliza;
"Niambie, endapo ukinunua zawadi kwa ajili ya kumpatia mtu, na mtu huyo akaikataa, Je zawadi hiyo inabaki kuwa ni ya nani?" 

Kijana ule alionyesha kushangaa kuulizwa swali hilo ambalo hakutegemea.
"Zawadi hiyo itabakia kuwa ya aliyenunua zawadi hiyo" Alijibu kijana yule.
Buddha akatabasamu na kumwambia,
"Upo sahihi. Na ni sawa na hasira yako. Kama ukiwa na hasira kwangu na sijajisikia vibaya wala kuharibu amani yangu ya moyoni basi hasira, chuki, na matusi yako yanabaki kwako. Wewe ndiye unayeshikilia hasira yako na sio mimi. Wewe nyiye unayeumia na hasira yako na sio mimi. Wewe ndiye ambaye hauna furaha, na sio mimi. Ulichofanya utakivuna matokeo yake wewe mwenyewe uliyetenda..." " Kama ukitaka kuacha kujiumiza kwa matendo yako, achilia hasira, chuki, hukumu, na ongeza upendo na amani. Unapochukia wenzio, wewe ndio unayekosa raha na sio wao. Na unapowapenda wengine wewe ndiye unayefurahia raha na amani ya upendo."

Kijana yule alitulia muda wote na kufurahia mafundisho ya mwalimu huyo. Akajibu
"Ni kweli mwalimu, nakuomba unifundishe njia ya upendo. Ningependa kuwa mwanafunzi wako."
Buddha akamjibu kwa ukarimu
"Mwanafunzi wangu ni kila anayependa kujifunza, nifuate uwe mwanafunzi wangu." 

Katika hadithi hii tunajifunza kuwa: Mtu akikusema vibaya au akikutusi usiumie. Yeye ndiye anayeteseka ndani mwake zaidi yako wewe. Jaribu kutomhukumu bali muone kama ndugu yako, naye anahitaji upendo, amani na mafundisho ya kweli ili ajitambue. Pia ni vyema kutoruhusu watu ambao wanakukosesha amani kwa maneno yao na matendo yao wasiondoe amani yako ya moyoni. Ukiweza kuwa mtulivu na mwenye amani wakati wote bila kukerwa na matendo ya watu au maneno ya watu unakuwa huru na mwenye amani ya ndani. Endeleza upendo!