Kuna Tofauti Gani Kati ya Wazo na Imani?
Posted by Unknown on 09:25 with No comments
KUNA TOFAUTI GANI KATI YA WAZO NA IMANI?
Wazo ni mtazamo au fikra inayobebwa akilini kutokana na uwezo wa kufikiria. Kutokana na hali ya KUFIKIRIA ambayo ni hali ya akili, mawazo au wazo huwepo. Kama kungekuwa hakuna kufikiria au akili ingekuwa haina uwezo wa kufikiria na kutafakari kusingekuwa na WAZO. Imani ni WAZO au msimamo uliokubalika, ambao mtu anaukubali kama ni kweli/uhalisia.
Mojawapo kati ya elimu bora kabisa katika kufahamu uhalisia wa maisha, ni kufahamu utofauti uliopo kati ya WAZO na IMANI na uhusiano wake kwa pamoja. Tofauti kati ya wazo na imani ni kuwa, unaweza ukawa na maelfu ya mawazo yaliyobebwa akilini lakini usiamini wazo hata moja. Wazo linaweza kuwa peke yake bila kuliamini. Lakini IMANI ni WAZO ulilolikubali kuwa ni uhalisia na unakubali kuwa WAZO hilo ni kweli. Wewe ndiye muamuzi wa kuamua ni mawazo yapi ni ya kweli na yapi sio ya kweli lakini pia kutokana na mazingira na mazoea huweza pia vikachangia kukufanya ukubali mawazo fulani (japokuwa utaona ni freewill yako lakini bado vitu vya nje ambavyo vinaweza kuadhiri mtazamo wako bila wewe kutambua hilo).
Imani huanza kama WAZO, Imani hapo mwanzo lazima ianze kama wazo, halafu baada ya wazo hilo kukubalika na kuaminika kama ni kweli basi huwa IMANI. Ufanano uliopo kati ya IMANI na WAZO ni kuwa unatumia UFAHAMU wako kuvitazama vyote hivi. Huwezi kuishika imani, huwezi kulishika wazo akilini, bali kwa kutumia ufahamu wako unaweza ukavitazama. Imani na Wazo. Utagundua kuwa havitazamiki kwa milango ya ufahamu (macho, pua, sikio, ngozi, n.k), bali unaweza kuvitazama kwa mlango mkuu wa ufahamu, ambao milango mingine ya ufahamu imekutania hapo. Ambapo mlango huo wa ufahamu ni akili.
Pia kuna HISIA, unaweza ukawa na mawazo mbalimbali lakini yakatofautiana uzito wa hisia na aina ya hisia. Hisia hujishikilia katika wazo. Hisia yenyewe kama yenyewe haiwezi kukaa peke yake akilini, lazima hisia iambatane na wazo. Unaweza ukawa na mawazo mbalimbali lakini kukawa hakuna hisia iliyojishikilia au kukawa na hisia ndogo lakini huwezi ukawa na hisia bila wazo lolote lililoshikana na hisia hiyo. Wazo likiwa na HISIA ni wazo ulilolipa kipaumbele sana. Ninaposema hisia ninamaanisha hisia ya aina yoyote. Iwe mbaya au nzuri, kubwa au ndogo, pana au fupi n.k
Kuna sehemu katika ufahamu wetu ambapo haitambui tofauti kati ya IMANI na UHALISIA, wazo lililokubalika kuwa ni kweli (IMANI) hukaa sehemu hii na kukubalika. Sehemu hiyo inashikilia mawazo yenye hisia zenye nguvu kubwa, na pia sehemu hiyo hushikilia uhalisia tunaouona katika maisha yetu. Sehemu hiyo haifahamu MAISHA yapoje, bali inatazama wewe unavyoyatazama maisha yapoje. Ndio maana sio kila wazo huathiri maisha yetu bali wazo lenye IMANI na HISIA kubwa, bila kujalisha ni aina gani za hisia na imani huathiri maisha yetu na jinsi tunavyoyatazama maisha. Hivyo kwa kuelewa hivi unaweza ukazidi kujichunguza na kujifahamu zaidi.

Asante.
0 maoni:
Chapisha Maoni