Kuacha Kuishi kwa Hasira na Lawama kila wakati.

Posted by Unknown on 20:00 with No comments
Hasira na malalamiko ni kama kunywa sumu, huku ukitegemea kumumkomesha adui yako kwa njia hiyo.  - Buddha


Hasira na Lawama hukuumiza wewe mwenyewe kwa ndani zaidi na sio unayemkasirikia au unayemlalamikia.
Msemo huo umetokana na kuwa Hasira humuathiri zaidi yule aliye na hasira kuliko yule anayekasirikiwa. Kushikilia hasira ni kama kushikilia kaa la moto. Tatizo wengi huona ni ufahamu wa kawaida lakini inahitaji umakini wa ndani sana kusoma maisha yanavyokufundisha. 

Fikra ya Malalamiko.

Hujawahi kukutana na mtu ambaye asilimia kuwa ya maisha yake anayatumia katika kulalamika? Utakuta wapo wanaolalamika kuhusu maisha, kazi zao, familia zao, marafiki zao, mazingira na mambo mengi. Wao katika kila jambo hutanguliza lawama. Wengi wao huamini kuwa maisha na kila kitu wanachokiona katika ufahamu wao ni kutokana na makosa ya mtu fulani au hali fulani. Wachache sana wenye ufahamu huo wanaoamini kuwa wana uwezo wa kubadili kila hali ambayo  wanaona ipo tofauti. Au pia wapo ambao wanaamini wanaweza kubadili hali lakini hawafahamu ni kwa namna gani. 

Sio sahihi kuweka lawama katika kila jambo linalotokea. Unapoweka lawama katika kila jambo linalotokea unajizuia kuelewa maana ya maisha. Kila wakati unaouishi una maana katika maisha yako. Hasa wakati huu uliopo, ukishindwa kutambua maana yake utajikuta unatafuta maana nje yako na maana ya maisha haitafutwi nje yako bali inatafutwa ndani yako. Tunapoweka mitazamo na lawama nje yetu kwa watu, kazi, maisha na mazingira tunajizuia kufahamu nafasi tulizonazo kubadili hali hizo na badala yake tunabakia tunaota bila kuamka katika uhalisia.

Uhalisia wa Hasira.

Kwanza ni vyema kujiuliza je Hasira ni muhimu? Je kuna faida yoyoe ya hasira? Hakuna faida yoyote ya hasira. Hasira inatokea pale tunaposhindwa kuongoza hisia na fikra zetu. Pale tunapokubali mawazo yatutawale ndipo hasira hutokea na kupata nguvu. Hasira inapokutokea kwanza jitambue kuwa una hasira na kubali kuwa una hasira. Wapo ambao wana hasira lakini wanaweza wakakataa kuwa wana hasira kwani hawajajichunguza au hawakubaliani na hali. Ukishajichunguza na kutambua uwepo wa hasira jaribu kuitazama hasira tu na sio kuiacha hasira ukutawale. Pale unapoitazama hasira bila kutumia maamuzi yoyote katika kuifuata na hasira nayo inaisha nguvu. Hasira hupata nguvu pale unaposhindwa kuichunguza kwa kila lakini ukiichunguza kwa kina yenyewe itaondoka na kuwa dhaifu kwani hasira haipendi itazamwe bali inapenda kutendwa bila kuchunguzwa. 

Jiweke Huru.

Kwani lazima kuwa na hasira na malalamiko maishani mwetu? Je hasira na malalamiko vinatokana na nini? Hutokana na kushindwa kuelewa uhalisia ulivyo (ujinga) na wasiwasi. Vyote hivyo havina umuhimu. Ni kama kubeba mawe na kutembea nayo. Unapoweza kutoshikiliwa na hasira na malalamiko unajiweka huru. Jambo au hali ikishatokea imetokea, hakuna kiasi cha hasira kinahohitajika katika kubadili hali au wakati uliopita na pia hakuna kiasi cha wasiwasi kinachoweza kubadili hali au kitu kilichopita tayari. Ni kukubaliana na hali iliyopo badala ya kujishikilia na wakati uliopita. Badala ya kulaumu panga mikakati ya kutumia nafasi yako kubadili jambo au hali. Badala ya kutumikishwa na hasira jenga upengo na amani na hasira nayo itashindwa.


Wasiwasi haukupeleki popote bali unakupotezea nafasi kufurahia wakati uliopo.