Badili Mawazo Yako Kubadili Fikra. Hatua Za Kubadili Mawazo.
Posted by Apolinary Macha on 14:23 with No comments
Mawazo na fikra za mwanadamu huumba maisha ya mwanadamu. |
Kuna
hatua mbalimbali ambazo mwanadamu anaweza akachukua pale anapotaka kubadili
mawazo. Kubadili mawazo au fikra ni muhimu sana kwani kama unapenda kubadili
maisha yako kuwa katika njia mbayo unapenda maisha yako yawe ni vyema kwanza
kubadilisha mawazo yoyote ambayo unayo kwani jinsi ulivyo au jinsi maisha
yalivyo kwako sio kutokana na uwezo wa nje yako bali ni kutokana na fikra na
mawazo yako. Mfano kama unatamani kuwa na roho nzuri ni vyema kuanza kuhisi
uwepo wa roho nzuri ndani yako, halafu amini uwepo wa roho nzuri upo na unaweza
kuutumia. Badala ya kuwa na hasira au chuki unaamua kujikumbusha kila wakati
kuwa unapaswa kuwa na roho nzuri. Cha ajabu ni kuwa tabia au mawazo yoyote
huweza kubadilika, na hubadilika pale unapoamua kweli na kujitolea kufanya
mazoezi. Mfano huo huo katika kuwa na roho nzuri, unaweza kujitolea katika kila
siku unafanya jambo lolote la kujikumbusha wema ulio nao moyoni, mfano kusaidia
au kujitolea muda, kitu, ushauri au chochote kumsaidia mwanadamu mwenzio katika
shida aliyo nayo.
Hatua
zifuatazo ni muhimu katika kubadilisha fikra au mtazamo wowote ulio nao ambao
unapenda uubadilishe.
1. Jizoeshe kurudiarudia mawazo, matukio au fikra nzuri.
Kila
unaporudia rudia wazo kichwani unajizoesha kuliamini na unalipa wazo hilo
nafasi ndani ya maisha yako. Mfano kama unaamini kuwa huwezi kufanya kitu
fulani, na kila saa unajisemea huwezi kufanya kitu fulani, basi unakaribisha
uwepo wa jambo lile katika maisha yako. Hivyo epuka mawazo au mazoea ya
kujisemea "siwezi kitu hiki" bali weka fikra na rudia rudia
kujisemea unaweza. Taaratibu utaona imani juu ya jambo unalolirudia inaongezeka
na unaona ni kama kweli, hapo inamaanisha imani yako inafanya kazi.
2. Hesabu furaha uliyo nayo na sio shida.
Pale unapopenda kubadili mawazo fulani, ni vyema kushukuru kwanza kwa ulichonacho. Maisha ni maajabu, unaweza ukawa unateseka na changamoto fulani kwa sababu unaikataa, na pale unapoikubali changamoto kama sehemu ya mafundisho ya maisha unakaribisha uwepo wa hali nyingine na ile hali ambayo unaiona ni changamoto inakuwa sio changamoto bali sehemu ya furaha ya maisha, furaha ya kujifunza changamoto zozote. Unaposhukuru kila jambo unakaribisha safari nyingine ya maisha.
3. Weka nia katika kubadilika.
Katika safari ya kutaka kubadili maisha yako inaweza ikakwama kwa sababu nia ni ndogo. Unapoweka nia katika kubadilika na kuwa na imani juu ya nia hiyo, unapelekea kutokea kwa mabadiliko. Safari yoyote inahitaji nia na imani.
4. Kuwa kiongozi wa mawazo yako.
Kila sekunde kuna wazo katika ubongo, ni jukumu letu kuchagua mawazo ya kuyapa kipaumbele akilini na kutoruhusu mawazo ambayo sio mazuri. Sisemi kwamba unaweza kuamua ufikirie nini, bali mwanadamu kuwa na mawazo au thoughts kichwani ni kawaida na huwa kila mwanadamu ana mawazo chanya na hasi. Mtu mwenye busara huchagua mawazo chanya daima.
Kumbuka:
Wewe peke yako ndiye kiongozi wa safari yako ya maisha, na wewe ndiwe mwenye
maamuzi juu ya mawazo yako, fikra zako na maamuzi yako.
0 maoni:
Chapisha Maoni