Mazoea ni Nini?

Posted by Apolinary Macha on 19:00 with No comments

Mazoea ni kama kifungo.
Jinsi mazoea yalivyo tunaweza kuyafananisha na Chombo cha Udongo.
Udongo hufinyangwa na kulainishwa kutengeneza umbo, umbo lile huchomwa na kuwa gumu. Likishakuwa gumu ni vigumu kufinyanga tena mpaka uvunje/ukisage chombo hicho cha udongo na ukichanganye na maji kilainike tena na ndio utengeneze umbo lingine ambalo unalitaka. Mawazo yako na fikra yako hutengeneza matendo yako. Pia jinsi unavyorudia rudia matendo yako na mawazo yako pamoja na fikra yako unazidi kuimarisha mazoea kupitia hivyo vyote. 

Mwanadamu ni kama vikaragosi(midoli ya maonyesho). Nyuzi ni mazoea yake, hisia zake, mawazo yake, fikra zake na milango yake ya ufahamu. VYote hivi huomuongoza kama vile kikaragosi kinachochezeshwa na nyuzi kwenye maonyesho.

Hata kama utakimbia kwenye pango au msituni au mbali bado tabia yako na  mazoea yako vitakufuata tu. Badala ya kuvikana unapaswa kuvitazama na kuvibadili. Safisha mazoea yako mabaya na sio uyakimbie.

Mazoea huanza katika hali ya wazo, baada ya kukaa kwenye ubongo kwa muda mrefu na kemikali za mwili huzoea. Hivyo mazoea huamia kwenye kemikali kutoka kwenye hali ya wazo. Mwili huyakubali mazoea na kemikali ya mwili hubadilika pale mazoea ya aina fulani yanapozidi kututawala. Inahitaji kujenga mazoea mazuri kuondoa mazoea mabaya tuliyojiwekea. Kama vile ilivyochukua muda kuzoea mwili na akili kuzoea mazoea mabaya ndivyo itakavyochukua muda mwili na akili kujenga mazoea mapya tunayoyataka katika maisha yetu.

Mawazo yako hupelekea matendo, matendo hupelekea mazoea, mazoea hupelekea kujenga sifa yako na sifa yako hujenga hali uliyonayo ya maisha yako kwa sasa.

Adui yako mkubwa ni mazoea yako mabaya. Hukufuata katika kila hatua ya maisha na hata baada ya maisha haya na maisha yajayo hukufuata daima kama kivuli chako kinavyokufuata kwenye mwanga. Ili kuachana na mazoea mabaya na kujiweka huru katika maisha yako inahitaji nia ya kwenye na nia yenye nguvu kuzidi nguvu ya mazoea. Nia ikiwa ni duni basi hutaweza kushinda mazoea yako bali mazoea yako yatakushinda. Ni vyema kujenga mazoea bora na taratibu yataanza kujengeka na kuondoa mazoea mabaya ya zamani. 

Mazoea mabaya ni Hatari katika Maisha.

Kila zoea linajenga sehemu yake kwenye akili. Sehemu hii inakua kubwa kwa jinsi unavyozidi kuipa nafasi. Maisha yako pia huchangiwa na mazoea yako. Mazoea yako mazuri na mabaya hujenga maisha yako. Kila mmoja ana uhalisia wake kutokana na mazoea yake. Mazoea sio kitu cha kawaida au kitu cha kupuuzia bali mazoea yana nafasi kubwa katika maisha yetu. 

Hata mafanikio ya maisha yanakuja kwa kujijengea mazoea ya aina fulani. Mfano mazoea ya bidii katika kazi, mazoea ya kuwa mkweli, mazoea ya kutochukua mali zisizo zako, mazoea ya kusema ukweli, mazoea ya kutotumia vitu vibaya kama pombe na kadhalika vyote hivi ni mazoea ambayo yanaweza kupeleka mbele mafanikio ya maisha yako. Hivyo mazoea yana nafasi kubwa katika mafanikio ya maisha yetu na katika kuipata furaha ya kweli.

Kama unavyoweza kujizoesha mazoea mabaya na ndivyo ilivyo kwenye kujizoesha mazoea mazuri. Unaweza kujizoesha mazoea mazuri na kuyazoea kama ulivyokuwa unazoea mazoea mabaya. Ni kuyapa mazoea mazuri kipaumbele na ukajikuta una mazoea mazuri yenye manufaa katika maisha yako.

Kupitia milango yetu ya fahamu tunaona, tunasikia, tunanusa, tunagusa,na tunaonja. Milango hii ya ufahamu kutumia akili yetu tunavyotafsiri experience tunaweza kujijengea mazoea. Mfano unaweza kujijengea mazoea ya kutazama kitu fulani tu, mazoea ya kupenda sauti fulani, mguso fulani, ladha fulani na pale tunapozidisha mazoea na kushikiliwa sana navyo basi mazoea hutokea. 

Utumwa wa akili unakuja kwa kuzoeshwa kuwa na mazoea ya aina fulani na kushindwa kutafakari ni kwanini una mazoea hayo. Wengi hawajitambui aina ya mazoea waliyo nayo na hivyo ni hatari sana kwani hawajitambu. 

Ni vyema kujifahamu, kurekebisha mazoea yako kama vile mfanya biashara anavyorekebisha bidhaa zake pale anapooona sio nzuri. Tunapaswa tujifahamu na tujitambue ili tufahamu undani na kilichopo ndani yetu. Kama hakina umuhimu ni vyema kukitoa na kujijengea mazoea na matendo yenye umuhimu. Ni vyema kuacha mazoea yasiyo na umuhimu na mazoea yanayokurudisha nyuma kimaendeleo. Jenga mazoea mazuri kila siku na utaona mabadiliko yake katika maisha yako ya nje.