Aina za Watu kutokana na Hasira zao.

Posted by Apolinary Macha on 04:00 with No comments


Kuna aina tatu za hasira za watu, au unaweza kusema kuwa kuna aina tatu za watu. Ambapo aina hizo za watu ni kutokana na hasira waliyonayo. Aina hizi za watu ni;
  • Watu wanaochora kwenye mwamba,
  • Watu wanaochora kwenye udongo/ardhi,
  • Watu wanaochora kwenye maji. 

Watu wanaochora kwenye Mwamba:

Hawa ni wale ambao hasira ikiwajia inakaa ndani yao kwa muda mrefu. Kama vile unapochora mwamba inachukua muda sana kufutika. Mpaka upepo, maji na hali ya hewa kubadilisha mchoro uliopo kwenye mwanga basi hata aina hii ya watu hasira yao inachukua muda kuondoka na wanateseka nayo bila kujijua.

Watu wanaochora kwenye udongo/ardhi.

Aina hii ya watu wenye hasira nao wanapata hasira, na hasira ikiwaingia haikai muda mrefu sana. Kama vile uchorapo kwenye udongo, mchoro utafutika lakini hautakaa sana.

Watu wanaochora kwenye maji;

Hawa ni wale ambao hasira ikiwaingia haikai, kwani wanaitambua hasira pale inapokuja lakini hawajishikilii nayo. Hasira inakuja na kupita papo hapo. Kama vile ilivyo vigumu kuchora kwenye maji basi ni vigumu pia kuwa na hasira kwa aina hii ya watu.

Utajifunza kuwa hakuna mwanadamu ambaye hana hasira, hasira inakuja kama vile mawazo yanavyokujaga. Ndio maana katika aina hizo za watu hatujasema kuwa kuna aina ya watu wasio na hasira kabisa. Tunachopaswa sio kutokuwa na hasira kwani ni vigumu kutokuwa na hasira, bali tunapaswa kuitambua hasira inapokujia, na kuhakikisha hasira hiyo haikuongozi bali wewe ndiye kiongozi wake. Usikubali hasira ikutawale, usikubali kufanya maamuzi kwa hasira.


Kuishikilia hasira ni sawa na kushika kaa la moto kwa kumrushia mtu, wakati na wewe pia unaungua nalo.