• Karibu Katika Blog Hii

    Blog Hii imelenga mafundisho mengi ya maisha katika safari ya mwanadamu Kujitambua na Kuamka

    Soma Zaidi
  • ONDOA VIPINGAMIZI VYA KUFIKIA MALENGO YAKO

    Anza kusema HAPANA kwa vitu ambavyo vinakuzuia kufikia malengo na ndoto zako za maisha. Matendo yanayokupotezea muda wako, marafiki wabaya, watu ambao maisha yao yanaweza kukupeleka pabaya, stress, hofu, matendo yanayoichukiza Nafsi yako.

    Fahamu Zaidi
  • Fahamu Jinsi Ya Kufanya Meditation

    Akili ya mwanadamu ina uwezo mkubwa sana kuliko anavyoichukulia. Mwanadamu akiweza kutumia ufahamu wake vyema, akaweka umakini kwenye akili yake, na kutambua nguvu ya imani na utambuzi wake anaweza kuwa mtu mkubwa sana

    Soma Zaidi

Jumatano, 23 Oktoba 2019

Kufikia malengo ya mbali, kunaaza na malengo haya haya madogo tuliyonayo kwa sasa.



Watu wengi wamekuwa na mawazo na malengo yanayofanana: 
“Kufanya mambo makubwa maishani, kufanya shughuli zenye manufaa kwenye jamii, mafanikio, pesa, familia, mali n.k.”

Pia kutokana na malengo haya utakuta kuna anayewaza
“Nikiwa CEO, nitafanya maamuzi yenye manufaa kwenye kampuni”
“Nikiwa na Biashara nitatenga fungu kidogo kusaidia watu”

Hivyo tunaishi maisha yetu tukiwa tunatamani kuwa katika hali mbalimbali ili kufanya mambo yenye manufaa kwenye jamii. 

Lakini mtazamo huu ni mzuri, japo una changamoto zake. Kwa maana ya kwamba, tunakuwa na mawazo kuwa mpaka uwe fulani…ndio utafanya mambo fulani… hali hii inatusahaulisha kuwa hata kwa muda huu ambao upo katika hatua yoyote bado unaweza kufanya mambo makubwa kama vile ambapo ungekuja kuwa hapo baadae. 

“Usisubiri kuwa CEO ndio uwe unafanya maamuzi ya msingi kwenye kampuni, usisubiri uwe na pesa ndio usaidie wenye shida, usisubiri uwe na pesa ndio uanze kufanya mazoezi, unaweza kuanza chochote hata sasa katika nafasi hii hii uliyonayo." 

Katika maisha, mambo madogo tunayoyafanya ndio msingi mkubwa katika maisha yetu. Furaha ni matokeo ya juhudi ndogondogo unazofanya katika maisha yako kila siku. Kila hatu uliyopo unaweza kufanya jambo dogo na kwa ukubwa. Pengine bado unapendelea kuwa na mambo makubwa, lakini kumbuka hata katika hali hii ndogo unaweza kufanya mambo yaliyo na msingi kabla ya kusema usubiri mpaka baadae ndio utaanza kuyafanya. Chochote unachofanya sasa kina msingi mkubwa katika maisha yako. Ukiwa na uelewa hii utazoea kufanya jambo wakati wowote, kwa hali yoyote na kwa ukubwa kutokana na kujenga mazoea sahihi mapema. 

Alhamisi, 10 Oktoba 2019

Changamoto na vikwazo vya Maisha


"Jifunze kutazama changamoto za maisha katika mtazamo tofauti"

Vikwazo na changamoto mbalimbali katika maisha ni hali ambayo huwepo kwa kila mtu. Ukitazama dunia kwa upande mwingine au kwa upande wa uhalisia utagundua kuwa kila kiumbe, vitu, wanadamu n.k vinapata changamoto fulani.

Chukulia mfano wa ukuaji wa mbegu: Mbegu inapoanza kuota na kukua hupitia changamoto mbalimbali. Lakini cha ajabu kupitia changamoto hizo mbegu hutumia changamoto hizo kujiboresha na kujiimarisha na hatimaye mbegu huota, hukua na kuzaa mbegu nyingine ambazo nazo zinapitia changamoto hizo.

Hebu jiulize, maisha yangekuwa hayana changamoto ungeimarika?
Changamoto hukupa nafasi ya kujipima, kutazama vitu katika hali tofauti ambayo bila changamoto usingeona hivyo, husaidia kujua njia za kuepuka changamoto hizo na kukuimarisha katika ubunifu wa maisha. 

BADALA YA KUACHIA CHANGAMOTO ZA MAISHA ZIKUTESE, TUMIA NAFASI HIYO KUJIIMARISHA. 



Jumatano, 10 Julai 2019

UPENDO - Njia Sahihi ya Kujitambua Na Kuishi Vyema.

Ishi kwa Upendo, Upendo wa Kujijali, Kujali wanadamu Wengine,
Kuheshimu kila kiumbe hai na kila kisicho Hai.
Upendo ni hali iliyofundishwa tangu enzi na enzi. Kila imani ulimwenguni inazungumzia kuhusu umuhimu wa upendo. Pia kila mtu anafahamu kuwa upendo ni kitu muhimu kwa mwanadamu. Mwanadamu anaweza akaishi bila mali, utajiri, sifa, lakini hawezi kuishi bila upendo. Ni dhahiri kuwa hata kama una kila kitu bila upendo unahisi hujakamilika. Upendo hukupa amani na faraja. 

Kutokwepo kwa upendo kunachangia maovu mengi na kupelekea watu kwenda njia ambazo sio sahihi. Upendo ni kinga na dawa ya matatizo mengi yanayomsumbua mwanadamu. Bila upendo huwezi kuwa salama kwani utaishi kwa wasiwasi wa kudhurika kwani hakuna anayekupenda. 

Walimu wa kale wamefundisha kuwa UPENDO ni suluhisho la maovu mengi. Ki ukweli ukiwa una UPENDO hautaweza kumkosea mwanadamu mwenzako, na vitendo kama vile Chuki, Hasira, Tamaa na Ubinafsi huondoka kwani badala ya mtu kujijali yeye mwenyewe kwa mapenzi ya UBINAFSI basi hataweza kuishi na wengine.



Fikiria UPENDO ulivyo na nguvu. Upendo huunganisha roho na nafsi za watu. Upendo ni gundi inayoziunganisha nafsi zetu. 


Nafsi zetu hutambua Upendo, na kwa kupitia Upendo nafsi zitu zinakua na Kujitambua zaidi
Upendo sio tu uliozoeleka wa Jinsia mbili tofauti, upendo tunaouzungumzia hapa ni Universal Love, Upendo juu ya Ulimwengu na vyote vilivyopo, Upendo kwa wanadamu wengine bila kujali umri, jinsia, kabila, nchi, au imani/dini. Upendo juu ya mazingira, mimea, mito, milima na kila kitu. Ukiweza kuishi kwa kutazama upendo mkuu kama wa yule Aliyepelekea uwepo wa vyote hivi utaweza kuona maisha ni furaha na upendo huchochea furaha.

Ki ukweli ukiwa na upendo kwako wewe binafsi, upendo kwa wanadamu wengine na upendo wa kwa kila kinachokuzunguka utaishi kwa haki, na amani kabisa. Hutaweza kujidhuru wala hutaweza kumdhuru mwenzako kabisa.

Sio tu upende anayekupenda bali penda wote, kwa asiyeonyesha upendo kwako naye mpende. Sio umpende kwa malengo binafsi bali kutoka moyoni na itakusaidia daima. Penda bila kujali utapendwa au utalipwa bali penda na jizoeshe kupenda na kujali wanadamu wenzako. 


Alhamisi, 23 Mei 2019

Kujitambua ni Hatua




Katika kutambua mzizi wa matatizo yetu, tabia zetu, maisha yetu na ukweli wa maisha, kujitambua ni jambo moja la msingi sana. Mwanadamu hata akitambua kuna sayari ngapi, jua ni nini, nyota zote, na viumbe vyote; bila kujitambua mwenyewe, hawezi kuwa na hekima sahihi. Na pia kujitambua ni kitu kigumu, kujifahamu na kuona uhalisia wako inahitaji juhudi sana. Ijapokuwa inahitaji juhudi, ni jambo la muhimu sana kwenye maisha yako. Itakusaidia kuishi na watu, kutenda yaliyo sahihi, kuwaza yaliyo sahihi na kuwa na hekima katika maisha yako. Mtu anayejitambua na kufahamu kwa kina nini maana ya maisha kwake, tayari anakuwa amepiga hatua kubwa. 

Lakini katika kujitambua kunahitaji kutoa mawazo ya watu kwa jinsi wanavyokuelewa. Inahitaji kujitenga na vile ambavyo havina manufaa kwako, kufahamu akili yako vyema, kufahamu mawazo yako vyema. Na hii ni kwa hatua moja baada ya nyingine. 

Kujitambua ni kitendo cha hatua na hakina mwisho. Ni safari isiyo na mwisho. Kujifahamu vyema katika kila wakati uliopo, kuwa makini na akili yako na matendo yako, kuwa makini na mitazamo yako na kuishi katika njia sahihi inayokutenga na mabaya. Kufanya hivyo kutapelekea kuishi katika hekima, kuacha mabaya, kuwa mnyenyekevu, mwema, na kuishi katika kusudi sahihi la uumbaji. 

Ijumaa, 10 Mei 2019

Uhalisia wa Furaha na Mateso katika Maisha



Maisha ni fumbo kwa kila mmoja wetu, na kila mwanadamu anaishi kwenye ulimwengu wake katika maisha yake. Fumbo la maisha ni kubwa na haijawahi kutokea mwanadamu ambaye ameweza kutoa mwanga kuhusiana na fumbo la maisha na jinsi ambavyo falsafa mbalimbali zimekuwa zikielezea. Ni fumbo ambalo tangu maelfu na mamia ya miaka iliyopita mwanadamu amekuwa akiwaza na kujiuliza kuhusiana na maisha ni nini. Ugumu wa swali hili ni kuwa kila mwanadamu anatafsiri kivyake na imani na falsafa ni nyingi na kila mmoja ina wafuasi wake. Unapokuwa falsafa ina wafuasi ni lazima kuwa kila mfuasi ameguswa na elimu hiyo na kuna sababu ya yeye kufuata maelekezo hayo na kujifunza kuhusiana na elimu hiyo au elimu mbalimbali. Yafuatayo ni mambo machache ambayo nimekuwa nikitafakari kuhusiana na furaha na mateso katika maisha yetu wanadamu:

Furaha katika maisha

Kila mwanadamu anaitafuta furaha! Tunapokuwa tunasoma shuleni ili kufaulu mitihani ni kwa sababu kufaulu ni furaha, kupata kazi nzuri ni furaha, kuishi sehemu nzuri ni furaha, kuwa na vitu vizuri ni furaha, kuwa na familia nzuri ni furaha, kuwa na afya ni furaha, kushinda ushindani ni furaha, kuwa na amani ni furaha, n.k. Kila tunachofanya tunafanya ili tuwe na furaha. Kila jambo ambalo tunaliwekea jitihana ni kuwa na furaha na kupunguza mateso na taabu za dunia. Furaha katika maisha yetu ni sehemu ya muhimu sana na ndio maana tangu tulipozaliwa tulianza kwa kujifunza kulia kwa ajili ya kuashiria kutopenda hali fulani na tulijifunza kufurahi kuonyesha hali nzuri; kabla ya kujua kuongea mwanadamu anajua kutofautisha furaha na mateso/maumivu katika maisha. Kila jambo tunalotenda ni kwa sababu ya kupenda kufikia furaha fulani.

Maisha yana mateso yasiyoepukika

Japo katika maisha yetu sisi wanadamu, tunajitahidi kuifikia furaha fulani lakini pia kwa upande mwingine hakuna mwanadamu ambaye ana furaha 100%. Bado kuna mateso ambayo yapo katika maisha na hayawezi kuondoka kamwe. Mwanadamu lazima azeeke, magonjwa mbalimbali, maumivu, kuishi na watu ambao wanatukosesha furaha, miili kuzeeka, majanga ya mvua, vimbunga, matetemeko, wanyama wakali na viumbe ambavyo hatupatani navyo mfano nyoka, simba n.k. Bado mwanadamu lazima ajitume ili kuishi vyema, lazima kuteseka kupata kile ambacho tunataka, na pia kuna mengi ambayo sisi kama wanadamu hatuwezi kuvipata. Maisha yana mateso yasiyoepukika.

Ukitafuta furaha kwa njia ambayo sio sahihi utapata mateso na hutovuna furaha sahihi

Chunguza katika maisha utaona kuwa mwizi hana furaha, muongo hana raha, mtu anayependa kuzini kuna taabu ataipata au anaipata katika maisha yake tofauti na mtu asiyefanya hayo. Mtu anayependa kulewa sana, kutumia madawa ya kulevya, kuvuta sigara, kupenda wanawake, kuua watu, kupigana, n.k vyote hivi huleta FURAHA YA MUDA MFUPI, na pia huleta taabu na mateso baadae. Wanadamu wanatofautiana jinsi ya kuitafuta furaha. Kuna njia sahihi za kuitafuta furaha ambazo ni njia zisizodhuru mwanadamu mwenzako, na njia isiyodhuru afya yako, maisha yako au mazingira. Kuna njia mbalimbali za kuitafuta furaha, kuna mtu anaitafuta furaha kwa kulewa, kuna mtu anaitafuta furaha kwa kuzini na kupenda wanawake, yote ni kuitafuta furaha au raha fulani katika maisha.
Tangu uumbaji ulivyoumbwa, furaha iliwekwa katika mazingira ambayo ukiitafuta katika njia sahihi utaipata na ukiitafuta katika njia ambayo sio sahihi utapata pia mavuno yake. Ni kama asali kwenye ncha ya sindano.

Utofauti wa maisha

Maisha yapo tofauti kwa kila mwanadamu. Wanadamu wanatofautiana sana kwa namna ambayo wanayaishi maisha yao, mateso na furaha wanazopitia. Kuna wanadamu wanaoishi kwenye taabu sana na kuna wengine wanaishi kwenye raha. Sio kwa sababu maisha hayana usawa, maisha yana usawa. Kwa wale wanaofahamu sheria ya KARMA, inasema kila mwanadamu anaishi katika maisha ambayo yeye mwenyewe ndio amepelekea kuyaishi. Inawezekana amesababisha kuishi kama alivyo sasa katika maisha haya au inawezekana katika maisha yaliyopita kabla ya haya kuna aliyotenda na kupelekea kuishi maisha haya. Na pia matendo ya sasa ndio muamuzi wa maisha yanayofuata. Kila hali ambayo mwanadamu anapitia ni kwa ajili ya kujifunza na kurekebisha makosa yake. Hakuna mwanadamu mkamilifu na ndio maana ni mwanadamu. Ukishakuwa mwanadamu inamaanisha kinachopaswa ni kujifunza na kujirekebisha maisha yetu. Mwanadamu ndiye kiumbe pekee anayejua ufahamu wa juu zaidi katika maisha na ulimwengu kwa ujumla. Pia ndiye kiumbe peke yake ambaye anajitambua. Jinsi tunavyowaza, matendo yetu, maneno yetu na fikra zetu ndizo zenye maamuzi ya maisha yetu tunayoyaishi.

Nini cha kufanya katika mateso na raha za maisha?

Kama hapo awali inavyoonyesha kuwa kwenye maisha kuna raha na shida. Kila analofanya mwanadamu ni kujifunza na kufahamu maisha kwa ujumla na pia kuitafuta furaha (katika maisha haya au maisha yajayo baada ya kifo). Kila mwanadamu ni dereva wa maisha yake, na kila mwanadamu anavuna fikra yake na matendo yake. Nini cha kufanya ili tuweze kuishi kwa furaha?

Kwanza ni kutambua kuwa kuna furaha ambayo inaweza kupatikana mfano kufanya kazi kwa bidii na kusimamia biashara zako vyema kwa ajili ya kupata kipato ambacho kitakusaidia kujikimu na kupata mahitaji ya muhimu kama sehemu nzuri ya kuishi, familia nzuri na mahitaji mazuri.

Pili, kuna ambavyo ni nje ya uwezo wetu katika kuwa na furaha. Mfano ni lazima mwanadamu afariki, watu wako unaofahamiana nao wanaweza kufariki, unaweza kuumwa ugonjwa wowote, unaweza kupata janga ambalo ni nje ya uwezo wako. Bado mwanadamu anazeeka, anakufa, anaumwa n.k Vyote vipo nje ya uwezo wetu na kila mwanadamu anapitia mateso fulani ambayo hana dawa ya kuyaondoa mateso hayo. Ni vyema kutambua hilo na halipingiki kabisa.

Tatu, ili kuwa na furaha katika mambo ambayo ni nje ya uwezo wako kama kuumwa, kifo, uzee; kwanza ni kutambua kuwa mateso duniani yapo, na kuna mateso ambayo ni nje ya uwezo wetu. Mateso haya hayaepukiki bali yanahitaji uwezo wako wa kutambua kuwa furaha inatoka akilini na sio kwenye hali uliyonayo. Unaweza kuwa na mateso yasiyoweza kuondoka wala kutibika na bado ukawa na furaha.

“Furaha katika maisha tunaitafuta, lakini pia kwenye maisha kuna mateso yasiyoepukika. Mateso haya ni sehemu ya maisha na mwanadamu anapaswa kujifunza kuitafuta furaha ndani mwake kabla ya kuitafuta nje yake.” 

Jumanne, 7 Mei 2019

Badili mawazo yako katika kuibadili fikra na Hatua za kubadili mawazo

Njia za Kubadilika



Mawazo na fikra za mwanadamu huumba maisha ya mwanadamu. Fikra ulizonazo juu ya maisha yako, mwili wako, mitazamamo yako ni muhimu sana kwani huweka uhalisia katika maisha yako. Pale unapoamini jambo fulani, kuna nguvu unaikaribisha katika imani yako ya moyoni. Ndio maana ni vyema kuwaza mawazo/fikra nzuri kwa husaidia kuwa na mawazo chanya ambayo yatakusaidia katika mitazamo na maisha yako kwa ujumla. Ni vyema kila siku asubuhi kuamka na kushukuru kwa kuamka salama, kuwa na mawazo na fikra nzuri na kutoruhusu mawazo mabaya kukutawala. Epuka mawazo ambayo ni adui kwa mwanadamu mfano tamaa mbaya, mazoea mabaya, ubinafsi, choyo, uadui, chuki n.k ambavyo hunyonya nguvu yako ya asili.



Kuna hatua mbalimbali ambazo mwanadamu anaweza akachukua pale anapotaka kubadili mawazo. Kubadili mawazo au fikra ni muhimu sana kwani kama unapenda kubadili maisha yako kuwa katika njia mbayo unapenda maisha yako yawe ni vyema kwanza kubadilisha mawazo yoyote ambayo unayo kwani jinsi ulivyo au jinsi maisha yalivyo kwako sio kutokana na uwezo wa nje yako bali ni kutokana na fikra na mawazo yako. Mfano kama unatamani kuwa na roho nzuri ni vyema kuanza kuhisi uwepo wa roho nzuri ndani yako, halafu amini uwepo wa roho nzuri upo na unaweza kuutumia. Badala ya kuwa na hasira au chuki unaamua kujikumbusha kila wakati kuwa unapaswa kuwa na roho nzuri. Cha ajabu ni kuwa tabia au mawazo yoyote huweza kubadilika, na hubadilika pale unapoamua kweli na kujitolea kufanya mazoezi. Mfano huo huo katika kuwa na roho nzuri, unaweza kujitolea katika kila siku unafanya jambo lolote la kujikumbusha wema ulio nao moyoni, mfano kusaidia au kujitolea muda, kitu, ushauri au chochote kumsaidia mwanadamu mwenzio katika shida aliyo nayo. 




Hatua zifuatazo ni muhimu katika kubadilisha fikra au mtazamo wowote ulio nao ambao unapenda uubadilishe. 


1. Jizoeshe kurudiarudia mawazo, matukio au fikra nzuri.


Kila unaporudia rudia wazo kichwani unajizoesha kuliamini na unalipa wazo hilo nafasi ndani ya maisha yako. Mfano kama unaamini kuwa huwezi kufanya kitu fulani, na kila saa unajisemea huwezi kufanya kitu fulani, basi unakaribisha uwepo wa jambo lile katika maisha yako. Hivyo epuka mawazo au mazoea ya kujisemea "siwezi kitu hiki"  bali weka fikra na rudia rudia kujisemea unaweza. Taaratibu utaona imani juu ya jambo unalolirudia inaongezeka na unaona ni kama kweli, hapo inamaanisha imani yako inafanya kazi.


2. Hesabu furaha uliyo nayo na sio shida.


Pale unapopenda kubadili mawazo fulani, ni vyema kushukuru kwanza kwa ulichonacho. Maisha ni maajabu, unaweza ukawa unateseka na changamoto fulani kwa sababu unaikataa, na pale unapoikubali changamoto kama sehemu ya mafundisho ya maisha unakaribisha uwepo wa hali nyingine na ile hali ambayo unaiona ni changamoto inakuwa sio changamoto bali sehemu ya furaha ya maisha, furaha ya kujifunza changamoto zozote. Unaposhukuru kila jambo unakaribisha safari nyingine ya maisha.


3. Weka nia katika kubadilika. 


Katika safari ya kutaka kubadili maisha yako inaweza ikakwama kwa sababu nia ni ndogo. Unapoweka nia katika kubadilika na kuwa na imani juu ya nia hiyo, unapelekea kutokea kwa mabadiliko. Safari yoyote inahitaji nia na imani. 


4. Kuwa kiongozi wa mawazo yako.


Kila sekunde kuna wazo katika ubongo, ni jukumu letu kuchagua mawazo ya kuyapa kipaumbele akilini na kutoruhusu mawazo ambayo sio mazuri. Sisemi kwamba unaweza kuamua ufikirie nini, bali mwanadamu kuwa na mawazo au thoughts kichwani ni kawaida na huwa kila mwanadamu ana mawazo chanya na hasi. Mtu mwenye busara huchagua mawazo chanya daima. 



Kumbuka: Wewe peke yako ndiye kiongozi wa safari yako ya maisha, na wewe ndiwe mwenye maamuzi juu ya mawazo yako, fikra zako na maamuzi yako. 



Jumatatu, 29 Aprili 2019

Tumia Fikra kidogo na hisia zaidi.


Osho quote Osho Swahili
Toka nje ya kichwa chako na ingia kwenye moyo wako, fikiria kidogo na ongeza hisia Zaidi – Osho

Ulishawahi kushikiliwa na akili? Au mawazo yako? Mfano badala ya kuweza kusuluhisha tatizo au jambo lililopo akilini unashindwa na badala yake akili ndio inazidi kuzidisha matatizo?

Kuna watu husema kuwa unavyozidi kulifikiria jambo ndipo unazidisha mawazo juu ya jambo unalofikiria, kumbuka akili inapenda kuwaza, unapopeleka wazo lolote kwenye akili ndipo unazidisha tatizo na sio kusuluhisha. Akili itazidi kuunganisha matukio, kukuambia kuna hiki na hiki na siku zote fahamu kuwa akili ina hofu. Akili inaogopa lakini siku zote moyo hauogopi. Moyo hauwezi kujua hofu bali akili ndiyo inayotambua hofu. Unapoona una hofu juu ya jambo lolote sio moyo wako umeona hivyo bali ni akili/fikra yako ndio ipo hivyo.

Ni vyema badala ya kutumia akili sana kuwaza, tumia na moyo kuhisi. Ni vigumu sana kujua hisia ya moyo na siku zote unapojaribu kutaka kufahamu moyo unataka nini akili huwa inakuzuia na inaweza kukudanganya kuwa moyo unahisi hivi kumbe sio kweli.

Roho zetu ndio zinatuunganisha na malaika mlinzi wetu na Muumba wetu, ukisikiliza roho inataka nini ufahamu kuwa hiyo ndio sauti ya ndani ambayo inamwelekeza kila mmoja wetu.

Muda utakaoweza kuusikiliza moyo unataka nini na akili nayo itatulia na itauheshimu moyo na maamuzi yake. Kumbuka maamuzi yaliyotoka kwenye nafsi ni ya muhimu na kuzingatia. Hutusaidia kufanya maamuzi mazuri hata tusipotambua mbeleni kuna nini.